Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkapa aacha alama Lushoto

7135afb860e616925a4fe77ceb8f8f2c Mkapa aacha alama Lushoto

Mon, 27 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA miaka 14 ya maisha ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa (81) katika Kijiji cha Mkuzi-Migambo Kata ya Migambo wilayani Lushoto mkoani Tanga alifanya mambo mengi ya kukumbukwa katika sekta za kilimo, mazingira, afya, elimu na miundombinu.

Mzee Mkapa aliweka makazi wilayani Lushoto baada ya kustaafu urais. Alianza kutafuta eneo la makazi huko mwaka 2001 hadi 2003, na baada ya kumaliza ujenzi, alihamia Januari mwaka 2006.

Kijiografia Wilaya ya Lushoto ni moja kati ya wilaya nane mkoani Tanga inayopatikana kwenye safu ya milima ya Usambara.

Wilaya hiyo kwa upande wa Kaskazini inapakana na Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, upande wa Mashariki inapakana na Wilaya ya Korogwe na Mkinga, upande wa Magharibi inapakana na nchi ya Kenya.

Hali ya hewa ya Lushoto ni baridi kali isipokuwa kipindi kifupi wakati wa kiangazi kuanzia Oktoba hadi Februari.

Uoto wa asili Lushoto ni misitu ya miti ya asili, katika wilaya hiyo kuna miinuko, miteremko na kona kali. Mwishoni mwa wiki mwandishi wa habari hii alifanya mahojiano na watu kadhaa waliokuwa karibu na Rais mstaafu Benjamin Mkapa wilayani humo.

DC January Lugangika Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, January Lugangika alisema mzee Mkapa alikuwa ni sehemu ya maendeleo katika wilaya hiyo katika sekta za elimu, afya, mazingira, kilimo na miundombinu ya barabara.

Alisema Mkapa alitoa mchango mkubwa hasa katika sekta ya afya na kupitia taasisi yake ya Benjamin Mkapa Foundation amejenga nyumba saba za waganda katika vituo vya afya vya Makanya, Gare, Bumbuli na Mlalo. Katika elimu, alisema mzee Mkapa alitoa misaada katika Shule za Sekondari Mazinde Juu, Mkuzi Juu na alitoa wazo la kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya Migambo ambayo sasa ina kidato cha nne katika kata ambayo alikuwa anaishi.

Kiongozi huyo pia alisaidia ujenzi wa Shule ya Msingi Kwezinga kwa kupeleka wafadhili wanaoitwa Good Neighbours waliosaidia kumalizia ujenzi wa jengo la utawala la shule hiyo.

“Mimi Mkuu wa Wilaya nasema tumepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa na mchango mkubwa wa maendeleo ya Lushoto katika sekta za afya, kilimo ambapo ameanzisha shamba darasa nyumbani kwake na wananchi wanakwenda kujifunza namna ya kilimo bora.

“Vile vile alitoa wazo la ujenzi wa barabara ya Lushoto- Mkuzi-Mlola yenye urefu wa kilometa 10 katika kiwango cha lami,” alisema.

Mbunge mstaafu, Shabani Shekilindi Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Lushoto (2015-2020), Shabani Shekilindi alisema mzee Mkapa kwa upande wake, alikuwa ni mshauri wa masuala ya kisiasa na uongozi.

Alisema mara nyingi alipokuwa anakwenda Lushoto alikuwa akimuita na kumuuliza kuhusu changamoto za kisiasa na ubunge alizokuwa akikabiliana nazo na kumshauri namna ya kuzitatua. “Marehemu licha ya kuwa ni Rais mstaafu, pia alikuwa ni mpigakura wangu katika jimbo langu, kwangu alikuwa ni nguzo muhimu, mshauri wangu na kiungo kwa upande wa maendeleo jimboni kwangu,”alisema.

Diwani, Kata ya Migambo-Mkuzi Diwani wa Kata ya Migambo-Mkuzi (CCM), Paulo Kiluwa Twaakyondo ambako Mkapa ana makazi huko anasema mzee Mkapa alikuwa kila anapofika Lushoto, alikuwa akimuita na viongozi wengine, kufahamu hali ya kisiasa wilayani humo na kuchangia mambo ya maendeleo ya kata hiyo.

Anasema katika kata hiyo, hakukuwa na shule ya sekondari lakini tangu alivyokwenda kiongozi huyo, aliwaita na kuwaeleza waanzishe shule ya sekondari ya kata ya Migambo.

Twaakyondo alisema, mzee Mkapa alitoa mchango wa fedha na vifaa vya ujenzi kama mwanakijiji na si Rais mstaafu.

Uongozi Chuo Kikuu Sekomu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Askofu Sebastian Kolowa (SEKOMU) ambaye kwa sasa ni Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edward Bagandanshwa alisema Mkapa alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la chuo hicho lenye wajumbe 10.

Chuo hicho kilichopo Lushoto, kinamilikiwa na Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT/DKMS). Profesa Bagandanshwa anashughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri.

Alisema Mkapa atakumbukwa na chuo hicho kwa mambo makuu mawili likiwemo la kukubali ombi la kuirudisha iliyokuwa Shule ya Sekondari Kongwe ya Magamba iliyokuwa inamilikiwa na kanisa hilo.

Serikali iliitaifisha mwaka 1970. Baadaye, Dayosisi hiyo katika mawazo ya kuanzisha chuo kikuu ikaigeuza shule hiyo kuwa kampasi B.

Alisema jambo la pili ni kuwa sehemu kubwa ya ushauri wake akiwa Mwenyekiti wa Baraza la la Ushauri alikuwa muwazi kwani aliongea ukweli bila ya kupindisha maneno na kilichobaki ni wao kuamua kufanya au kuacha. “Katika kutambua mchango wake, chuo chetu tumejenga ukumbi mkubwa wa mikutano na tukaamua kuupa jina lake ambao unajulikana kama ‘Benjamin Mkapa Auditorium,”alisema.

Aliongeza: “Vile vile alianzisha kampeni ya utunzaji mazingira ambapo kupitia chuo cha Sekomu, tumeweza kupanda miti milioni moja wilayani hapa,” alisema Profesa Bagandanshwa.

Padri Joseph Kikoti, Paroko wa Mkuzi Padri Joseph Kikoti, Paroko wa Kanisa la Roma, Parokia ya Mkuzi anasema Mkapa alikuwa ni muumini mzuri kila alipokuwa anakwenda Lushoto.

Alisema alipokuwa akienda Lushoto kufanya ibada alikuwa akipewa nafasi ya kuzungumza na waumini na jambo kubwa alilokuwa akisisitiza ni kudumisha amani.

“Wakiwa akiwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, alitutaka kuwaombea wananchi wa nchi hiyo pamoja na yeye katika kazi yake hiyo aliyokuwa amepewa ya usuluhishi,” alisema. Pia alikuwa akitoa mchango mkubwa katika ujenzi wa kanisa jipya katika parokia hiyo ambayo ujenzi wake unaendelea.

Chanzo: habarileo.co.tz