Katavi. Mkandarasi wa kampuni ya LGNA aliyekuwa akijenga barabara ya Mkokwa-Mnyagala halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi amefukuzwa kazi kwa kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati.
Mbali na kufukuzwa anashikiliwa na Takukuru kwa agizo la mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Saleh Mhando.
Katika ziara yake ya kushtukiza Machi 19, 2020 alichukua hatua hiyo na kuwapa onyo Mamlaka ya Barabara mijini na vijijini (Tarura) na kuwatahadharisha mameneja wa Tarura kuhusu mkandarasi huyo kutofanya kazi vyema lakini hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yake.
"Fedha zipo tangu mwaka 2019, umesaini mkataba Oktoba 2019, mpaka sasa hakuna ulichokifanya tofauti na kumwaga kifusi mradi unatakiwa ukamilike April 9,2020 zimebaki siku ngapi? Tumeshindwa kupitisha vifaa kwenda kujenga kituo cha afya, wananchi wanaendelea kupata shida wakati rais anatoa fedha ili kuboresha huduma katika jamii.
Mkurugenzi wa kampuni ya LGNA, Michael Kessi baada ya kuhojiwa kuhusu kuchelewa kukamilisha mradi huo amesema ameshindwa kutekeleza kwa wakati kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Pia Soma
- Corona yabadili utaratibu wa abiria kupanda mabasi mwendokasi
- VIDEO: Wakuu wa shule waliowafukuza wanafunzi kuepuka corona waonywa
- Jimbo la California latangaza amri ya kukaa ndani kudhibiti corona
Kwa upande wake kaimu meneja Tarura wilaya ya Tanganyika, Maila Richard amesema licha ya kutoa maelekezo kwa mkandarasi huyo anakaidi na kuendelea kujenga kinyume na utaratibu unaotakiwa.
"Kazi ameifanya kinyume na utaratibu tulivyohitaji sisi kimkataba have grade siyo sahihi, anatakiwa ainue tuta baada ya hapo amwage kifusi lakini hafanyi hivyo, wiki iliyopita nilimpa maelekezo. Jumatatu akaendelea tena, nimemwandikia barua kifusi hiki akitoe afuate utaratibu unaotakiwa ili wananchi waweze kupita na yeye aendelee na kazi zake,
Baadhi ya wananchi, Joseph Emmanuel na Charles Ng'wandu wamesema hali hiyo inawaathiri kiuchumi kutokana na magari kukwama mara kwa mara, waendesha pikipiki na baiskeli nao wanapata usumbufu.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 1.5 inatakiwa kujengwa kwa Sh74 milioni ambapo imefikisha wakandarasi watatu wanaofukuzwa bila kupata malipo kwa kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati.