Serikali imetoa miezi miwili kwa kampuni tanzu ya Shirika la Umeme (Tanesco) ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDC) kufuatia kusuasua kwa miradi ya kusambaza umeme katika vijiji 139 wenye thamani ya Sh36.8 bilioni katika wilaya tano za Mkoa wa Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema leo Jumamosi Januari 28, 2023 kwenye kikao cha kupokea taarifa ya maendeleo ya mradi wa kusambaza Umeme Vijijini (Rea) kilichohusha wawakilishi wa wabunge, wajumbe wa bodi Rea makao makuu na wasimamanizi wa mradi huo.
Homera amesema kuwa amechoshwa na utendaji na wa kampuni hiyo na kuunga mkono agizo la Waziri wa Nishati, Januari Makamba la kutoa muda wa miezi miwili na kutaka wajitathimini kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo ambayo inaleta malalamiko kwa wananchi.
Amesema mkataba wa mradi ni miezi 18 ambao utekelezaji wake ulianza Agosti 2021 na unatakuwa kukamilika Februari, 2023 huku vijiji 19 vimewashwa na 35 vimefungwa mashine ya transfoma kwa ajili ya hatua za awali huku 104 havijafikiwa na mradi.
“Waziri wa Nishati, Januari Makamba ametoa muda wa miezi miwili kwa kampuni ya ETDCO kujitathimini na kuhakikisha vijiji 35 vinawashwa umeme huku vijiji 104 watoe maelezo, kama serikali imekaa nao vikao kadhaa vya kuwaelekeza ambavyo havijaleta matokeo mazuri huku miradi ikisuasua,” amesema Homera.
Amesema ufike wakati kampuni za Serikali zinazopewa tenda za miradi ya wananchi kutekeleza kwa wakati siyo kusubiri kuvutana na viongozi huku akiweka bayana kutokubalina na uzembe wa usimamizi wa mradi huo usipokamilika kwa wakati wahusika watakamatwa na kuchuliwa hatua.
“Kikao hiki cha mwisho kwa Kampuni ya ETDCO tayari Waziri wa Nishati, Januari Makamba amekaa nanyi na kuwalekeza kwa sasa tunahitaji taarifa za kila wiki kuhusiana na hatua za utekelezaji wa mradi huo,” amesema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (Rea) kutoka wizarani, Frolian Haule amesema wamelazimika kufika Mkoa wa Mbeya ili kujua changamoto za mkandarasi wa kutokamilisha miradi kwa wakati kabla ya hatua kuchukuliwa ikiwepo kusitisha mkataba.
Haule amesema kampuni hiyo imekuwa na changamoto nyingi za utekelezaji wa miradi licha ya kufanya nao vikao kupitia wizara jambo ambalo hata Waziri Makamba hajarishishwa.
“Tumekuja Mbeya watendaji wa Rea na bodi kufanya kikao cha pamoja baina ya Mkuu wa Mkoa na mkandarasi wa kampuni ya ETDCO kwani utendaji wake hauridhishi ili kumsikiliza na kabla ya Wizara ya Nishati hatujafanya uamuzi kwani hata Waziri Makamba hajaridhishwa na ndio maana tupo hapa,”amesema.
Mkandarasi wa Kampuni ya ETDCO, Mhandisi Mustapha Himba amesema mpaka sasa wamefunga mashine za umba (transfoma) kwa vijiji 35 kati ya hivyo 19 umeme umewashwa vingine wanasubiri vifanyiwe ukaguzi ili kuruhusu kuwashwa huku 104 havijafikiwa na mradi.
“Mh Mkuu wa Mkoa Katika vijiji 139 tumewasha 19 pekee na mkataka ulikuwa wa miezi 18 hivyo tuko nyuma ya muda, hivyo tunarajia kuongeza kasi ya vijiji vingine 30 mpaka ikifika mwezi Aprili 2023,”amesema.