Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkandarasi Rea apewa siku 15 kuwasha umeme

48570 PIC+WAZIRI

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kasulu. Waziri wa Nishati, Medard Kalemani amempa siku 15 mkandarasi wa kampuni ya Jiangsu Etern Co Ltd wa Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) kuhakikisha anawasha umeme katika kijiji cha Ruhita kilichopo wilayani hapa.

Kalemani amebainisha hayo leo, Machi 25, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ruhita akidai kuwa kijiji hicho ni cha muda mrefu na haiwezekani kikose umeme mpaka leo.

Amesema Serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi wanapata umeme na kuharakisha maendeleo katika maeneo yao.

"Serikali inampa siku 15 mkandarasi kuhakikisha anawasha umeme katika kijiji chenu na kuripoti kila siku asubuhi katika ofisi ya mwenyekiti wa kijiji, lengo ni kwenda kwa kasi," amesema Waziri Kalemani.

Aidha Waziri Kalemani amewataka wananchi wa kijiji hicho kuweka umeme katika nyumba zao kabla ya Julai mwaka huu, kwani ni nishati muhimu kwa maendeleo yao.

Amesema Julai, mwaka huu, ataenda kufanya ziara ya kukagua maendeleo katika mkoa huo na akienda nyumba ambayo haina umeme na anafuga mifugo kama kuku, watauza ili waweze kumuwekea umeme katika nyumba yake.

Amewataka wananchi kulipa kidogo kidogo gharama za umeme kwa Sh27,000 na kwamba atakapomaliza watamuwekea umeme wake.

"Mradi wa Rea hauna fidia kwa wananchi hivyo niwaombe wananchi kutoa maeneo yao kupitishia nguzo za umeme kwani ni kwa manufaa yao na hazitumii eneo kubwa," amesema Waziri Kalemani.



Chanzo: mwananchi.co.tz