Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkandarasi 'Government City Complex' ahimizwa kukamilisha mradi kwa wakati

F75d288318a9e1599fa6f07c1b287d38 Mkandarasi 'Government City Complex' ahimizwa kukamilisha mradi kwa wakati

Tue, 27 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MENEJIMENTI ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imemuagiza mkandarasi Kampuni ya Mohammed Builders anayejenga jengo la kitega uchumi la 'Government City Complex' kukamilisha na kukabidhi mradi huo ifikapo Desemba 30 mwaka huuu.

Agizo hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipoongoza timu ya menejimenti kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa katika mji wa serikali eneo la Mtumba jijini hapa.

"Nimekuja na timu ya menejimenti ili kuangalia maendeleo ya mradi, hivyo nakukumbusha mkandarasi mradi huu kuwa kwa mujibu wa mkataba wetu unatakiwa kuisha Desemba 30 mwaka huu na bahati nzuri yeye anasema hana kikwazo chochote hivyo unataka mradi ukamilike kwa muda uliopangwa," alisema.

Mafuru alisema mradi huo umejengwa katika mji wa serikali yalipo makao makuu ya serikali eneo la Mtumba ili kuwezesha kutoa huduma katika eneo hilo.

"Lengo la mradi huu ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati yeye anapambana kujenga ofisi za serikali hapa Mtumba, sisi kama jiji tunapambana kuhakikisha huduma ambazo zitakosekana kwenye maeneo mengine zinapatikana katika jengo hili. Jengo hili lina awamu nne.

"Hii ni awamu ya kwanza ambayo tumekuja kuishuhudia ikiwa inaelekea ukingoni, nimetaarifiwa kuwa awamu hii ujenzi wake umefikia asilimia 60."

Mafuru alitumia fursa hiyo kuwaalika wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kutembelea mradi huo na kuweka miadi ya kupanga katika jengo hilo.

"Mradi huu utakuwa na maeneo ya biashara, maduka makubwa ya biashara, sehemu za taasisi za kifedha. Lakini pembeni tunajenga ukumbi mkubwa wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 500 ili kurahisisha shughuli zote za serikali kufanyika katika eneo hili.

"Eneo hili la mji wa serikali litakuwa na wageni wengi ambao watakaokuwa wakihitaji huduma za serikali, mabalozi, wawekezaji na watumishi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi," alisema na kuongeza kuwa awamu ya kwanza itagharimu Sh bilioni 18.

Naye Mhandisi Rayson Merinyo kutoka Kampuni ya Mohammed Builders alimhakikishia Mkurugenzi wa jiji kuwa mradi huo utakabidhiwa ifikapo 30 Desemba, 2020.

Alisema kuwa katika kufanikisha kukamilika kwa mradi huo, ujenzi utafanyika usiku na mchana ili kuharakisha mradi huo.

Chanzo: habarileo.co.tz