Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkaguzi Mahita aeleza mbinu aliyotumia kumkamata mshtakiwa

Msuya Bilionea.jpeg Mkaguzi Mahita aeleza mbinu aliyotumia kumkamata mshtakiwa

Wed, 28 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkaguzi wa Polisi, Mahita Omari Mahita ameieleza Mahakama kuwa walifanikiwa kumtia mbaroni mshtakiwa wa pili, Revocatus Everist Muyella katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, baada ya askari mmoja kumuomba lifti amkampeleka hadi kituo cha polisi.

Mahita alieleza mbinu hiyo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Mbali na Revocatus maarufu kama Ray, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018, Miriam Mrita ambaye ni mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya.

Aneth aliuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada-Kigamboni, Dar es Salaam ikiwa ni miaka mitatu tangu kuuawa kwa kaka yake Bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Akiongozwa na mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali Mwandamizi, Generose Montano, Inspekta Mahita ambaye kwa sasa anafanya kazi ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Morogoro alidai alimkamata mshtakiwa huyo wa pili Agosti 19, 2016 jijini Arusha.

Alieleza wakati huo alikuwa akifanya kazi ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wilayani Arusha, akiwa na cheo cha Mkaguzi Msaidizi na kwamba siku ya tukio alipewa maelekezo hayo na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, George Katabazi.

Alieleza mkuu wake huyo alimweleza kuwa mtuhumiwa Revocatus anadaiwa kufanya mauaji ya Aneth na kwamba anaishi Arusha na anatumia gari aina ya Range Rover ya zamani, toleo la kwanza.

Alidai kuwa aliingia mitaani kumsaka na muda wa jioni, eneo la mnara wa Mwenge karibu na ofisi za CCM mkoa akiwa na askari wa doria, aliliona gari hilo likiegshwa.

Hivyo, alimjulisha kamanda wake ambaye alimweleza atafute mbinu nzuri ya kumkamata.

“Miongoni mwa askari niliyokuwa nao ni pamoja na Koplo Abdallah, alikuwa anafahamiana na Ray (mtuhumiwa), hivyo nilimwambia ashuke aende akaombe lifti kwa Revocatus, ili amshushe kituoni,” alieleza na kuongeza kuwa yeye alitangulia kituoni na akawaelekeza askari getini kuwa gari hilo likifika walifungulie liingie.

Hata hivyo, alidai gari hilo lilifika kituoni hapo na likaegeshwa nje ya kituo, Koplo Abdalla na mtuhumiwa wote wakashuka ndipo akajitambulisha kwake na akamuuliza majina yake, naye akajitambulisha anaitwa Revocatus maarufu Ray.

“Nikamwambia yuko chini ya ulinzi, kuna tuhuma zinazodai kuwa amefanya tukio la mauaji Dar es Salaam. Hivyo nikatoa maelekezo mtuhumiwa huyo awekwe mahabusu na aliwekwa akasubiri mpaka ofisa upelelezi afike.”

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano baina ya mawakili wa utetezi, Peter Kibatala na Nehemia Nkoko na Inspekta Mahita:

Wakili Peter Kibatala: Shahidi unamfahamu huyu dada (mshtakiwa wa kwanza, mjane wa Bilionea Msuya)?

Shahidi Mahita: Simfahamu

Kibatala: Wakati unakamatwa Ray, Revocatus alikuwa na personal properties (mali binafsi)?

Mahita: Hakuwa nazo.

Kibatala: Hakuwa hata na funguo za gari?

Mahita: Nimesema alikuwa na gari.

Kibatala: Simu zake tatu?

Mahita: Siwezi kujua

Kibatala: Yeye anasema alikuwa na simu tatu na wallet ikiwa na Dola 450

Mahita: Si kweli.

Kibatala: Mna ugomvi na wewe mpaka atunge stori?

Mahita: Sina

Kibatala: Pia anasema ulichukua Sh60,000

Mahita: Si kweli

Kibatala: Pia mlikwenda kumpekua nyumbani kwake?

Mahita: Ni sahihi kabisa.

Kibatala: Mbona hukumwambia Jaji hilo?

Mahita: Nimeeleza nilichokifanya

Kibatala: Mlipata vitu gani?

Mahita: Sikumbuki

Kibatala: Mteja wetu anasema wewe na Afande David Mwanaya mlikwenda kumfanyia upekuzi saa 7:36 hivi usiku

Mahita: Mheshimiwa (jaji) si kweli

Kibatala: Kwa nini atunge?

Mahita: Si ni yeye mwenyewe ndio anaongea.

Kibatala: Eneo la tukio wewe ulikuwa ni shahidi huru?

Mahita: Waliokuwepo mashahi huru

Kibatala: Hawa mashahidi wawili walioshuhudia wakati wanatafutwa wewe ulishiriki?

Mahita: Mimi sikushiriki

Kibatala: Zaidi ya upekuzi na zoezi la kumkamata Revocatus, kuna kingine cha kiupelelezi ambacho unakijua?

Mahita: Mheshimiwa zaidi ya hayo hamna kingine.

Wakili Nehemia Nkoko: Iambie Mahakama ulivyokwenda kushudia huo upekuzi ilikuwa muda gani?

Mahita: Asubuhi

Nkoko: Asubuhi ya saa ngapi?

Mahita: Muda Sikumbuki

Nkoko: Kwa hiyo toka umemkamata mpaka mnakwenda kumpekuwa utakubakiana na mimi yale masaa ya kawaida manne hadi nane ya kisheria yalikuwa yamepita?

Mahita: Mheshimiwa kwa mujibu wa swali lake hakuna specific section (kifungu maalumu) ambayo imeweka limit (ukomo- muda wa kumfanyia mtuhumiwa upekuzi tangu kukamawa), kama unayofungua.

Nkoko: Anafungua sheria na kusoma moja ya vifungu vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kisha anauliza: sasa swali langu utakubakiana na mimi).

Mahita: Umekuja na sect hapa hiyo haijasema....

Nkoko: Mheshimiwa sasa mimi ngoja nikae chini, ili anifundishe sheria (anakaa).

Mahita: Katika hiyo section uliyoisoma haijaweka limitation ya kufanya upekuzi

Nkoko: Shahidi umeleta ushahidi wa nyaraka kuthibitisha kuwa Agosti 19, 2016 ulimkamata Revocatus Muyella na kumuweka kizuizini kituo cha Polisi?

Mahita: Mheshimiwa, labda asema nyaraka gani?

Jaji: Swali lake ni kwamba umetoa nyaraka?

Mahita: Mi sijatoa nyaraka Mheshimiwa

Nkoko: Tofauti na maneno yako matupu, una uthibitisho gani hapa mahakamani kama ulimkamata?

Mahita: Ushahidi nilioutoa hapa mahakamanai na nimemuona hapa kuwa ni yule pale.

Nkoko: Namuonyesha maelezo ya David Mwanaya (mpelelezi) kisha namaamuliza muda alioandika waliokwenda kumpekua mtuhumiwa kuwa inasomeka saa ngapi?

Mahita: 02:00 hours

Nkoko: Ambayo ni saa ngapi?

Mahita: Saa mane

Nkoko: ya muda gani?

Shahidi: Mimi sijui labda aliyeandika.

Kisha aliulizwa maswali na mwendesha mashtaka kusawazisha majibu ya maswali ya mawakil wa utetezi.

Montana: Umeulizwa kuhusu upekuzi, wewe jukumu lako lilikuwa nini?

Mahita: Jukumu langu lilikuwa ukamataji tu.

Montana: Umeonyeshwa hapa karatasi kuhusu muda wa upekuzi wewe unasemaje?

Shahidi: Siwezi kumbuka

Montana: Sasa kwako wewe upekuzi ulifanyika muda gani saa 8 usiku au asubuhi?

Mahita: Mheshimiwa Mimi upekuzi ulifanyika tarehe 20, sasa hayo mengine sikumbuki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live