Hakuna aliyedhani kama katika siku za hivi karibuni angeona tabasamu usoni mwa Anna Zambi, mwanafunzi aliyefiwa na wazazi na wadogo zake watatu.
Lakini alitabasamu! Tabasamu lake la matumaini liliwalifanya waombolezaji waliokuwapo nyumbani kwao Goba, jijini Dar es Salaam kutabasamu pia.
Binti huyu mwenye umri wa miaka 16 alitabasamu baada ya kukutana na msanii Mrisho Mpoto maarufu ‘Mjomba’ aliyemwambia, afute machozi kwa kuwa yeye ni shujaa.
Mpoto; Mimi ni nani?
Anna; Mjomba
Mjomba maana yake nini?
Anna; Kaka yake mama
Mpoto; Eheee mimi ni kaka yake mama, maana yake mimi ni mama, sawa eeh! Kwa hiyo futa machozi kwa sababu hauko peke yako. Tabasamu na sema ‘mimi ni shujaa’.
Na kweli Anna alitabasamu kutokana na maneno ya Mpoto aliyemtaka asema kwamba, yeye ni shujaa na atasimama kusaidia watoto wengine walioshindwa kutimiza ndoto zao baada ya kukutana na mambo magumu kwenye maisha yao.
Anna aliyekuwa anasoma Shule ya Sekondari Mother Theresia of Calata iliyopo Same mkoani Kilimanjaro inayoendeshwa na Jimbo Katoliki la Same, alifichwa taarifa za vifo hivyo ili afanye mitihani ya kidato cha nne.
Baba yake Lington Zambi, mama yake Wilfrida Lyomo Zambi na wadogo zake Lulu, Grace na Andrew walifikwa na mauti baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na mafuriko katika eneo la Gandeni mkoani Tanga.
Wazazi na ndugu hao walipoteza maisha Oktoba 26 wakati wakielekea shuleni kwa Anna kuhudhuria mahafali yake ya kidato cha nne.
Mpaka anamaliza mitihani Novemba 16, hakuwa na taarifa yoyote kuhusu kilichoikumba familia yake.
“Mkinisaidia nitasoma kwa bidi ili nami nije kuwasaidia wengine waliokumbwa na matatizo kama yangu,” anasema Anna.
Anna ametoa kauli hiyo baada ya Serikali kumpa matumaini ya kumsaidia kwa kumpa tiba ya kisaikolojia, kumsomesha na kumsimamia hadi atimize ndoto zake za kielimu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu aliahidi Serikali kusimamia masuala yote yanayohusu ustawi wa Anna.
“Pole nyingi kwa binti yetu Anna Zambi. Hili jambo ni kubwa mno kwa mtoto huyu. Inaumiza sana, Ninamuombea kwa Mungu ampe nguvu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
“Nasi Wizara ya Afya tukiwa na dhamana ya kusimamia ustawi na maendeleo ya watoto nchini, tunachukua jukumu la kuratibu na kusimamia psychosocial support ya mtoto huyu pamoja na masuala mengine yanayohusu ustawi wake,” anasema Waziri Ummy.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, John Jingu alipotembea familia hiyo alisema: “Huyu mtoto wetu ana ndoto. Bila shaka atafanya vizuri kwenye mitihani yake ya kidato cha nne, kwa hiyo Serikali tunachukua jukumu la kuratibu na kuhakikisha anafikisha ndoto zake”.
Anasema wamekubaliana kumpa tiba ya kisaikolojia hata huko mkoani Arusha alipokwenda kuishi na mama yake mdogo.
“Ningekuja na Waziri wangu lakini yupo mbali. Serikali yako ni mzazi wako. Serikali haitakuacha,” anasema Jingu.
Pia mbunge wa Bumbuli, January Makamba pamoja na wanakikundi wenzake wa kikundi cha RG Brothers juzi walifika nyumbani anapoishi Anna na kumpa maneno ya faraja.
“Kitu kikubwa katika msiba kama huu ni faraja, faraja ni kutembelewa na kuja kupewa pole na kuonyesha kwamba mtu hayupo peke yake,” anasema Makamba.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, anasema baada ya kuona hali hiyo atawashirikisha wanakikundi wenzake na kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kutoa msaada kwa mtoto huyo.
Daktari Fredric Doya anasema mtoto huyo anapaswa apumzike kwanza na aachwe apitie hatua zote za kupokea habari mbaya, kabla ya kuanza kupata ushauri wa kisaikolojia.
Anataja hatua hizo ni kukataa, hasira, kujiuliza maswali (kama taarifa husika ni za kweli) na kisha kukubaliana na hali halisi.
Dk Doya anasema wakati akipitia hatua hizo, ni vizuri akaendelea kupata nasaha za kiroho na kuongeza kuwa hayo yakifanyika ipasavyo atarejea katika hali ya kawaida.
Shule ilivyozuia taarifa
Mwakilishi wa wazazi wa watoto katika shule hiyo, Doya anasema baada ya msiba, uongozi wa shule uliwathibitishia utazuia mianya yote inayoruhusu taarifa hizo kuenea shuleni na kumfikia mtoto huyo.
Anasema wanafunzi walizuiwa kutowasha televisheni na kuhakikisha hakuna mawasiliano ya simu yanayowafikia wanafunzi.
Mtawa asimulia
Mlezi wa wanafunzi katika shule hiyo, Mtawa Mndeme anasema siku moja baada ya mahafali hayo akiwa amelala alisikia mtu akilia kwa sauti kubwa.
Akizungumza wakati akitoa salamu za rambirambi katika msiba huo, anasema sauti hiyo iliongezeka ambayo ilikuwa ya kupiga mayowe, hivyo aliamka na kwenda kuangalia kuna nini, ndipo alipomkuta Anna akilia akieleza kuwa amesoma miaka minne, lakini wazazi wake wameshindwa kwenda kwenye mahafali yake.
“Nilimwambia wazazi wengi wanaoishi Dar es Salaam wameshindwa kwenda katika mahafali kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha, kusababisha mafuriko,” anasema.
Mtawa huyo anasema linapotokea jambo, roho huwa zinawasiliana ingawa kwa macho ya kawaida unaweza usione.
Baba yake mdogo, Ibrahim Zambi alisema baada ya Anna kumaliza mitihani walimfuata shuleni ambapo aliuliza sababu ya kutomuona baba na mama yake.
Anasema walimwambia kuwa wanakusubiri nyumbani kwa kuwa kuna sherehe na kueleza kuwa kila mmoja alihofia namna gani mtoto huyo atapokea taarifa hiyo.
“Tulipofika umbali kama wa mita 100 toka ilipo nyumba ilibidi watu wanne, wanaume wawili na wanawake wawili wakampokee na hapo ndipo walipomweleza kuhusu kilichotokea,” anasema Ibrahim na kuongeza;
“Baada ya taarifa alilia sana, alishikiliwa hadi nyumbani akaenda kulala kwenye miguu ya bibi yake anayeitwa Anna Kamwela.”
Anna alikuwa akilia huku akisema: “Mbona mmeniacha peke yangu? Kwanini imekuwa hivi baba na mama? Mmeondoka hamjaniachia wadogo zangu ili niwalee, nitaishije peke yangu?”
Hakuna aliyehimili sauti iliyojaa maneno ya huzuni toka kwa Anna.
“Hata nikifaulu sitakuwa na furaha, nani nitamuonyesha matokeo yangu? Mdogo wangu Lulu matokeo yako ya darasa la nne niliyaona ila yangu hutayaona,” anazungumza Anna wakati akilia.
Hali hiyo ilisababisha waombolezaji kububujikwa na machozi, Mchungaji wa Kanisa la Moravian, Hance Mwakisoja aliyekuwa anaongoza ibada nyumbani alikatisha mahubiri na kuwataka waombolezaji kila mmoja asali, ili kumuombea mtoto huyo.
Wakati wote Anna alikuwa akipungia mkono picha za familia yake zilizokuwa zimewekwa mezani.
“Uliona wapi mtoto mdogo kama mimi anabebeshwa majeneza matano? Nilijua nikitoka shule nakuja kumlea mdogo wangu (Grace aliyekuwa na mwaka mmoja) kumbe ameniacha, oooh naumia mimi” alilia kwa huzuni Anna;
“Wadogo zangu niombeeni nami nije huko, maisha yaliyobaki nitaishi kwa tabu sana.”
Tangu kutokea msiba huo Anna alikuwa hajaambiwa chochote ili afanye mitihani, lakini wakati akilia alisikika akisema alihisi jambo baya hasa siku ambayo wazazi wake hawakutokea kwenye mahafari yake.
“Usiku ule niliamka nikaanza kulia mbona sijawaona? Kumbe mlikuwa mmeniacha nilihisi tu kuna kitu sio kawaida, baba na mama msije?” alisema.
“Tulimuacha apumzike mpaka saa nne, tukamuandaa kwa ajili ya ibada lakini tunamshukuru Mungu kwa sababu mtihani mkubwa ilikuwa ni namna gani atapokea taarifa hizo,” anasema.
Eneo jingine waombolezaji walijikuta kila mmoja akibubujikwa machozi ni wakati mtoto huyo alipokuwa akiweka mataji.
Alikumbatia misalaba ya wazazi wake huku kila mmoja akimuongelea maneno yake mithili kama wanamsikia.
“Baba yangu nisamehe, mimi ndio sababu ya nyie kufa, kama kusingekuwa na mahafari msingeniacha. Mmeondoka kwa ujinga wangu,” alizungumza Anna.
Alimpa pole mama yake alipofika kwenye kaburi lake akisema “Ulituzaa kwa uchungu tuje kukusaidia lakini ona mama, umeondoka na wadogo zangu nimebaki peke yangu.”
Kwa wadogo zake, Anna alisema alitamani kuwalea na kuwasaidia wasome kwa bidi huku akimtaja Ander aliyetamani kuwa Injinia kuwa ndoto zake zimezima kama mshumaa.