Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mjane atimuliwa kwenye nyumba ya urithi

Mjane Nyumba Mjane atimuliwa kwenye nyumba ya urithi

Wed, 27 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Faustina Kimamba mkazi wa Kijiji cha Mapili, Kata ya Ilela, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi, ameiomba serikali imsaidie kupata stahiki zake, alizochuma na marehemu mumewe, Josephat Kanyongo, anazodai amedhulumiwa na mtoto wake wa kumzaa.

Akizungumza hivi karibuni na HabariLeo Online, Faustina anasema aliishi na mume wake kwa miaka 20 na kupata watoto watano, lakini baada ya kufariki mumewe mwaka 2010, alikaa miaka mitatu na kupata mwanaume mwingine waliyepanga kuoana na kuishi naye.

“Jamii zetu hazikuwa tayari nilete mwanaume mwingine kuishi naye katika ile nyumba ya marehemu, hapo ndipo matatizo makubwa yalipoanza,” alisema.

Akisimulia kisa kizima, alisema baada ya ndugu wa marehemu mume wake kupata taarifa kuwa anataka kuolewa na mume mwingine, walimchukua mtoto wake wa pili, Agustino Josephat aliyemzaa mwaka 1993 na kumshawishi amfukuze kwenye nyumba, ndipo mtoto huyo alipotekeleza amri hiyo.

"Nilikuwa nikilalamika wale upande wa baba yake wanasema ukienda kumshitaki ni wewe na sisi, akifungwa huyo mtoto utazaa na sisi,"alisema na kueleza kuwa karibu miaka nane sasa ameshindwa kulalamika kwa kuhofia vitisho.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mlele, Finner Soka amesema watajitahidi kufuatilia changamoto ya Faustina na kuona namna ya kumsaidia, ili kupata stahiki zake na ikiwezekana kufikisha suala hilo katika vyombo vya sheria.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele, Theresia Irafay amemtaka mjane huyo kufika ofisini kwake, ili kuona namna wanavyoweza kumsaidia, huku akitoa wito kwa wananchi wengine kuviona vyombo husika pale wanapofanyiwa vitendo ya ukatili wa kijinsia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live