Mwanamke aitwaye Faustina Kimamba, mkazi wa Kijiji Cha Mapili wilayani Mlele mkoani Katavi ambaye ni mjane amefukuzwa na watoto wake kwenye nyumba na mashamba waliyotafuta na mumewe aliyefariki 2010, baada ya kuanzisha mahusiano na mtu mwingine.
Akisimulia kisa kizima cha tukio hilo, mjane huyo amesema alishawishika kuingia kweye mahusiano kutokana na hali ya kiuchumi, watoto wadogo na mwanume huyo alikuwa akimsadia huduma mbalimbali.
Akizungumza hivi karibuni, Faustina anasema aliishi na mume wake, Josephat Kanyongo kwa miaka 20 na kupata watoto watano, lakini baada ya kufariki mumewe mwaka 2010, alikaa miaka mitatu na kupata mwanaume mwingine wa kuishi naye.
“Hapo ndipo matatizo yalipoanza, jamii zetu hazikuwa tayari nilete mwanaume mwingine kuishi naye katika ile nyumba ya marehemu, hapo ndipo matatizo makubwa yalipoanza,” alisema.
Bi Faustina amesema mtoto wake wa pili kumzaa ndiye aliyemfukuza huku akimtupia maneno makali kwa kumuita malaya. "Mtoto wangu alikuja akaniambia mama nataka unipe godoro, nilipotoka nilikuta mtoto ameshabeba godoro, mimi nikaendelea kulala chini, badaye mtoto akaenda kujimilikisha mashamba, katika hekari 40 mimi alinipa heka 2, kwa kuwa nilikwenda kwa mtendaji wa Kata kulalamika,"alisema.
"Sehemu yoyote atakayouza, mtoto yeyote haruhusiwi kusema, nilikuwa nikizungumza wale upande wa baba yake wanasema ukienda kumshitaki ni wewe na sisi, akifungwa huyo mtoto utazaa na sisi," alisema.
Alisema baada ya kupokea vitisho hivyo, aliogopa kwenda popote na ndipo alifukuzwa yeye na baadhi ya watoto wake wengine kwenye nyumba ya marehemu mume wake.
Alisema sababu kubwa ya kufukuzwa ni yeye kupata mwanaume mwingine wa kuishi naye, lakini mtoto wake mkubwa na ndugu wa marehemu mume wake walipinga vikali kwa madai ni kinyume na mila zao.
Licha ya kuondolewa katika nyumba hiyo, muda mfupi baadaye alipata pigo lingine kwani yule mwanaume hakuendelea naye, hivyo akaamua arudi kwa wazazi wake.
Kutokana na hali hiyo, Faustina anasema baadhi ya watu wamemshauri asikae kimya, ndiyo sababu ameanza kupaza sauti na kuiomba serikali imsaidie angalau kurejesha baadhi ya mali ambazo bado hazijauzwa na mtoto wake, ikiwemo nyumba pamoja na mashamba, ili imsaidie kupunguza ukali wa maisha.
Mjane huyo ameelezea vitisho na maonyo makali aliyoyapata toka kwa ndugu wa mme yaliyompelekea kupata hofu na kuacha kufuatilia mali hizo huku akiishia kuendelea kutaabika kimaisha.
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mlele, Finner Soka watajitahidi kufuatilia changamoto ya Faustina na kuona namna ya kumsaidia, ili kupata stahiki zake na ikiwezekana kufikisha suala hilo katika vyombo vya sheria.
"Mahakama iamue kama alichuma mali na mume wake kwa miaka 20 moja kwa moja zile mali ni za kwake na watoto, haiwezekani mtoto akatoka akaenda kumfukuza mama yake.
"Kitendo cha mwanamke huyu kufukuzwa nyumbani inawezekana hakuwa na kauli kutokana na jamii kama hii, mume akifariki mwanamke haruhusiwi kuwa na uhusiano mwingine, ingawa mume akifiwa na mke wake jamii inaruhusu kuoa na kumleta palepale kwenye mji alioishi mke wake," alisema Finner.
Kwa upande wake, Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele, Theresia Irafay amekemea vitendo hivyo na kumtaka mhanga kufika ofisini kwake mara moja ili apewe msaada wa kisheria.
Irafay amemtaka mwanamke huyo kufika ofisini kwake, ili kuona namna wanavyoweza kumsaidia, huku akitoa wito kwa wananchi wengine kuviona vyombo husika pale wanapofanyiwa vitendo ya ukatili wa kijinsia.