WATU wanane wamekufa na wengine sita kujeruhiwa, akiwamo mjamzito baada ya basi dogo la abiria kuacha njia, kugonga wapita njia na kupinduka katika Barabara ya Uganda mjini Bukoba mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malim alisema jana kuwa basi hilo, Toyota Hiace lenye namba za usajili T471 DCG, lilikuwa likitoka Kemondo kwenda Bukoba Mjini.
Kamanda Malim alisema wakati likiwa kwenye mwendo mkali, mfumo wa breki uliharibika, likagonga watembea kwa miguu wawili kwenye Mtaa wa Rwamishenye na kufa papo hapo.
Alisema gari hilo lilipopinduka watu wengine watatu walikufa kwenye eneo la ajali na wengine watatu waliaga dunia kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa Kamanda Malim, baada ya gari hilo kupinduka juzi saa 1:40 usiku, lilitumbukia kwenye shimo.
Alisema Polisi wamemkamata dereva wa basi hilo, mkazi wa Kemondo, Ismail Rashid (37), kwa tuhuma za kuendesha gari hilo kwa mwendo kasi na kusababisha ajali.
Jana wananchi walikwenda kuitambua miili ya marehemu hospitalini hapo.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Riclain Ndostaini alidai wakati akiwa barabarani akienda nyumbani, alishuhudia basi likiwa kwenye mwendo wa kasi likamgonga mama mmoja na kufa papo hapo.
“Kuna mama mmoja kama vile alikuwa akitokea sokoni amevalia kitambaa shingoni ile anavuka tu barabara nikaona kwa macho yangu anagongwa na kufa na gari ilikuwa upande upande,” alidai Ndostaini.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa, Yustas Tibanga alisema walipokea miili ya marehemu sita wa awali na baadaye waliongezeka wawili. Alisema pia walipokea majeruhi sita walioumia usoni, mikono na kichwani.
“Majira ya saa mbili usiku tumepokea majeruhi wanne ambao wanapewa matibabu na timu ya madaktari, wapo walioumia usoni, kichwani na mikono, lakini pia na miili sita ipo chumba cha kuhifadhizia maiti,” alisema Dk Tibanga.
Mganga Mfawidhi katika hospitali hiyo, Dk Charles Kahigi aliwataja marehemu kuwa ni Dominick Kibuka (48), Reticia Gration (58), Raushati Khalfani (35), Rehema Abubakary (30), Johnson John (26) na Anchira Rweyendera (62).
Alisema marehemu wote walikuwa wakazi wa Bukoba Mjini, na kwamba miili miwili haijatambuliwa.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo aliyelazwa hospitalini hapo, Mektilida Angekile (19) alisema alikuwa a