Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miundombinu taka hatarishi kugharimu bil 11.5/- 

Plastic Recycling Miundombinu taka hatarishi kugharimu bil 11.5/- 

Sun, 29 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHILINGI bilioni 11.5 zinatarajiwa kutumika kuboresha miundombinu ya uteketezaji wa taka hatarishi zilizopo Kisarawe mkoani Pwani.

Mkurugenzi wa Taasisi inayohusika na ukusanyaji taka hatarishi mazingira (Tindwa), Maimuna Salum, alitoa taarifa hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Zanzibar.

Alisema kwa sasa taasisi hiyo inatoa huduma nchi nzima na kwamba katika Mkoa wa Dar es Salaam, wanahudumia taasisi zaidi ya 100.

“Tumepata ugeni ambao dhamira yao ni kujifunza kuhusu taka hatarishi. Kwa sasa kampuni inadhamiria kukuza teknolojia ya utekezaji wa taka na hivi sasa tunatarajia kuwa mfumo wa kuteketeza kemikali za maji na kemikali ngumu,” alisema.

Alisema mpango mwingine ni kujenga sehemu za kupokea taka mbalimbali na mfumo kwa ajili ya ukusanyaji na urejeshaji wa taka hatarishi zinazotoka hospitalini.

“Tuna mpango wa kuweka teknolojia kwa ajili ya kurejesha taka hizo na upande wa Zanzibar pia tutajenga, lakini si kubwa sana kutokana na eneo lake,” alisema.

Maimuna alisema changamoto iliyopo kwa upande wa Zanzibar ni kukosa eneo la uwekezaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Saada Mkuya Salum, alisema wanaenda kufanyia kazi changamoto ya eneo la kujenga mitambo ili kudhibiti taka hatarishi.

Alisema kwa upande wa Zanzibar, ipo changamoto kubwa kwani wakati mwingine taka hatarishi zinazagaa baharini hivyo ujenzi wa taasisi hiyo utakuwa na msaada mkubwa.

“Zanzibar sasa ni changamoto Hospitali ya Mnazimoja wakati mwingine miundombinu inaharibika hali hii ukienda baharini unakuta sindano zimemwagwa, hivyo changmoto ni kubwa tunahitaji mitambo hii kufanya uteketezaji,” alisema Waziri.

Alisema kadiri uchumi wa nchi unavyokua, na uzalishaji wa taka hatarishi unaongezeka hivyo uzagaaji wake kuwa hatari hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ni sehemu ya utalii.

Chanzo: www.habarileo.co.tz