Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miti 1,500 yapandwa chanzo cha maji cha Mwitore

1d478b4d1a249b27c5d98cd28c4e36cb Miti 1,500 yapandwa chanzo cha maji cha Mwitore

Sun, 4 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BODI ya Bonde la Ziwa Victoria kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Kwibusye, wilaya ya Rorya mkoani hapa wamepanda miche ya miti ipatayo 1,500 kwenye chanzo cha maji cha Mwitore, ikiwa ni jitihada za kutunza chanzo hicho kiendelee kutoa huduma za uhakika za majisafi na salama kwa wanajamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga alitaka wananchi kuacha tabia ya kukata miti hovyo na kuchoma moto milimani ili kulinda vyanzo vya maji.

Alisema hivi karibuni Idara ya Maji iliwekeza zaidi ya Sh milioni 140 kutafuta maji kwani maeneo mengi yanayokabiliwa na ukosefu wa maji kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.

“Wafundisheni vijana wenu wajue kukata miti ovyo ni laana, waache kuchoma moto milimani, tutakayembaini amefanya hayo tutamchukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kulipa faini," alisema Odunga.

Ofisa wa Maji, Mwita Mataro alisema chanzo cha maji cha Mwitore ni chemichemi ambayo awali ilikuwa hatarini kupotea lakini ilinusurika kwa jitihada za serikali na wadau mbalimbali kuweka uzio ili kuzuia uharibifu uliokuwa unafanywa na wanyama.

Alisema hatua ya upandaji wa miti katika eneo hilo ni muendelezo wa jitihada za wadau wakiwemo Bodi ya Bonde la Ziwa la Victoria, kulinda chanzo hicho kwa boresha mazingira yake kwani kinatoa huduma kwa wananchi wasiopungua 2,000

Mmoja wa wakazi wa Kwibusye, Mariam Chacha alisema awali walikuwa wanatumia maji na wanyama wa porini pamoja na mifugo, hali iliyohatarisha afya za wananchi.

Alisema ujenzi wa uzio umenusuru afya zao kwani sasa hakuna mnyama wa aina yoyote anayeingia katika chanzo hicho cha maji.

“Ilikua ni uchafu binadamu kutumia chanzo cha maji na wanyama. Hata zuio la ukataji miti lilikuwa gumu kwa sababu eneo lilikuwa wazi muda wote tofauti na sasa ambapo kumezungushiwa uzio. Tutashirikiana na serikali pamoja na wadau katika kuhakikisha chanzo hiki kinalindwaa muda wote," alisema.

Mkazi mwingine, Spora Charles, alisema kabla chanzo hicho kuboreshwa kwa kuwekewa uzio, upatikanaji wa maji ulikua shida hasa kipindi cha kiangazi kwani binadamu na wanyama wote walitegemea eneo hilo moja.

“Yaani unachota maji hapa, pale ng’ombe au mbuzi nao wanakunywa maji. Lakini tangu uzio uwekwe wanyama tunawachotea na kuwatengea nje ya uzio.”

Alisema wananchi wanashukuru jitihada zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama wakati wote na kuhaidi kutoa ushirikiano wa kutosha kulinda chanzo hicho.

Chanzo: www.habarileo.co.tz