Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita imebaini kasoro mbalimbali kwenye miradi 17 ya maendeleo yenye thamani ya Sh14.9 bilioni hali iliyosababisha baadhi ya miradi kutokamilika kwa wakati huku mingine ikijengwa chini ya kiwango.
Miradi iliyofuatiliwa ni pamoja na miradi 12 ya sekta ya elimu, afya na maji inayotekelezwa kwa fedha za Uviko 19 yenye thamani ya Sh 2.6 bilioni ambayo baadhi imebainika fedha kuisha wakati miradi haijakamilika na miradi mingine kuchelewa kuanza kutokana na zoezi la kutafuta wakandarasi kuchukua muda mrefu.
Akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita mkuu wa Takukuru mkoani hapa Leonidas Felix alisema baadhi ya miradi imebainika kuwa na vifaa vya ujenzi visivyo na ubora uliokusudiwa.
“Baadhi ya miradi inahujumiwa mfano kule Chato mkandarasi amewasilisha mabati 741 yenye thamani ya sh 19 milioni yako chini ya kiwango ndio maana nasema hatutembelei tu miradi, tunakagua tukiwa na wataalamu na hatuishii tu hapo wahusika waliofanya hujuma kama hizi wanachukuliwa hatua za kisheria,“ amesema Felix.
Felix alisema kwa kipindi cha miezi mitatu taasisi hiyo imegundua kasoro katika ukusanyaji na uwasilishaji wa mapato ya yanayokusanywa kwa mfumo wa POS katika halmashauri mbili za wilaya ya Geita na kusema taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Sh 61milioni kati ya sh 113milioni zilizokusanywa bila kuingizwa katika akaunti za halmashauri.
Advertisement Aidha kwa kipindi hicho cha miezi mitatu taasisi hiyo imepokea taarifa ya malalamiko 74 na kati ya hizo 61 zinahusu masuala ya rushwa huku serikali za mitaa zikiongoza kwa kuwa na malalamiko 37 kati ya 61 yaliyolalamikiwa.
Alisema katika kudhibiti taasisi hiyo imefanya chambuzi sita za mifumo ya viashiria vya rushwa ambapo katika ushuru wa madini ya ujenzi imebainika shughuli hizo kufanyika bila vibali na kukosekana kwa ukaguzi madhubuti wa magari yanayobebea madini ya ujenzi hivyo kuikosesha serikali mapato.
Katika uchambuzi kwenye sekta ya ujenzi na usimamizi wa miradi ya maendeleo na matumizi ya Force akaunti wamebaini kuwepo kwa usimamizi hafifu wa miradi kutoka kwa wataalamu.
Pia wananchi kutokuwa na uelewa, urasimu katika kukagua miradi pamoja na wakandarasi wanaopewa miradi kutokuwa na uwezo wa kutekeleza miradi.