MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla, ametembelea miradi mitatu ambayo ilielekezwa kusimama ujenzi wake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ummy Mwalimu, kutokana na kasoro zilizoonekana ambapo amesema muda wowote kuanzia sasa atatoa barua ya kuelekeza kuendelea kwa miradi hiyo
Miongoni mwa miradi hiyo ni Jengo la utalawa Manispaa ya Kinondoni linalogharimu sh Bilioni 2, Uwanja wa Timu ya KMC na Kituo cha Daladala cha Mwenge
Juni 20 mwaka huu, Ummy, alifikia uamuzi wa kusimamisha miradi hiyo baada ya kuikagua na kutoridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo kwani tangu ilipoanza hadi alipotembelea Juni 20,2021 ilikuwa imefikia asilimia 46 ya utekelezaji wake, licha ya kuongezewa muda.
''Sijaridhishwa na hatua za ujenzi wa stendi ya mabasi Mwenge, zipo sarakasi kwenye huu mradi zipo sintofahamu kubwa ili niweze kujiridhisha nasimamaisha ujenzi na naunda timu ya kuchunguza miradi yote mitatu stendi ya Mwenge, uwanja wa mpira pamoja na jengo la utawala wa Manispaa ya Kinondoni nataka kujiridhisha,'' alisema Ummy, Juni 20, 2021
Pia aliunda timu huru ya kuchunguza mikataba yote ya miradi hiyo ili kujiridhisha, ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi Mhandisi wa Manispaa Isack Mpaki
Hata hivyo, Makalla leo amesema kasoro zilizojitokeza zimerekebishwa na muda wowote kuanzia sasa atatoa barua ya kuelekeza kuendelea kwa miradi hiyo.
Aidha Makalla amewapongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kutekeleza miradi mikubwa kwa mapato ya ndani.