Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi 16 ya maji kuwaneemesha wananchi Tanga

Maji Miradi 16 ya maji kuwaneemesha wananchi Tanga

Thu, 30 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Tanga (RC), Adam Malima amesema miradi ya maji inayotekelezwa katika mkoa huo inakwenda kutatua changamoto katika maeneo yenye tatizo kubwa la upatikanaji wa nishati hiyo.

RC Malima ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 30, 2021 wakati wa uingiaji wa mikataba 16 ya miradi ya maji katika mkoa wa Tanga.

Amesema miradi 16 ya maji yenye thamani karibu ya Sh10 bilioni inakwenda kuimarisha ubinadamu wa Watanzania hasa katika maeneo yenye tatizo kubwa la upatikanaji wa maji mkoani hapa ni suala lenye msingi mkubwa kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi.

"Tumuunge mkono Rais wetu katika safari yake hii, miradi ya shule, afya, maji na mambo mengine makubwa anayofanya ni kwa ajili ya Watanzania,"amesema Malima

Malima amewataka wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo waisimamie vizuri huku wakiamini kwamba Serikali inatarajia miradi hiyo inaleta tija kwa wananchi.

Awali meneja wa mkoa wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Upendo Lugongo amesema miradi hiyo 16 itahusika katika wilaya saba katika vijiji 33 zenye idadi ya watu watakaonufaika wapatao 95,043 sawa na asilimia 3.9 ya wakazi wote wa mkoa wa Tanga.

Amesema katika miradi hiyo kazi zitakazohusika ni pamoja na kujenga matanki 20 ya maji yenye ujazo wa lita zipatazo 2,250,000 utakaokuwa na mtandao wa mabomba yenye urefu wa kilomita 230,006 na vituo vya kuchotea maji 235 ikiwemo uunganishaji umeme, ununuzi wa jenereta na pump.

Meneja huyo wa Ruwasa amesema katika ya miradi hiyo, mikataba saba fedha zake zimepatikana katika mfuko wa IMF zilizotokana na janga la Uviko-19 na fedha nyingine zimepatikana katika mfuko wa maji (NWF) na mfuko wa malipo ya fedha ( PbR).

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandila amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji wakizingatia kwamba kila mwaka kuna mabadiliko ya tabia nchi yanayoathiri maeneo mengi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live