Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Milonde waishukuru Serikali kukamilisha mradi wa maji

B0ef1d940544f07cf23996e9f2e9f96f Milonde waishukuru Serikali kukamilisha mradi wa maji

Mon, 19 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKAZI wa Kijiji cha Milonde kata ya Matemanga wilayani Tunduru, wameishukuru serikali kwa kukamilisha mradi wa maji ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2012 ambao umesaidia kumaliza kero ya muda mrefu ya maji safi na salama.

Mkazi wa kijiji hicho, Habibi Kassim amesema hapo awali walilazimika kuamka kati ya saa 10:00 na 11:00 alfajiri kwenda kutafuta maji katika vyanzo visivyo rasmi huku wakati mwingine wakikutana na wanyama wakali wakiwemo tembo na nguruwe pori.

Alisema kukamilika kwa mradi huo ni faraja kubwa kwao kwa sababu mbali na kumaliza kero ya muda mrefu, pia utachochea maendeleo ya wananchi wa kijiji hicho na kata mzima ya Matemanga.

Naye Rehema Awadhi ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Milonde alisema siku za nyuma walilazimika kwenda shule wakiwa wachafu kutokana na kukosekana kwa maji ambapo ameishukuru serikali kukamilisha mradi wa maji Milonde.

Hata hivyo, ameiomba Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa)kuongeza vituo vya kuchotea maji katika kijiji hicho ili kupunguza kero kwa watu kutumia muda mrefu kwenye vituo vilivyopo kwa ajili ya kupata huduma ya maji.

Alisema licha ya serikali kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ulioanza kujengwa miaka 12 iliyopita, bado kuna changamoto ya wananchi kukaa muda mrefu katika vituo vya kuchotea maji.

Alisema vituo saba vilivyopo havitoshi jambo linalosababisha watu kukaa kwa muda mrefu na wakati mwingine kutokea kwa vurugu ya kugombea maji na hata kupoteza muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Tunduru, Primy Damas alisema vituo vilivyojengwa kwa ajili ya kuchotea maji katika Kijiji cha Milonde ni 12 ambapo kwa sasa vinavyofanya kazi ni saba.

Alisema hali hiyo imetokana na kushindwa kupata kibali cha kupitisha mabomba kutoka kwenye tangi kwenda katika vituo vya kuchotea maji kutoka kwa Wakala wa Barabara Tanzania(Tanroads), kwani miundombinu ya mradi huo ni lazima ipite katikati ya barabara .

Mradi wa maji Milonde umetengewa Sh 160,467,626 na hadi sasa fedha zilizotumika ni Sh 111,128,500 ambapo mradi huo umekusudia kuhudumia wananchi zaidi ya 3,000.

Alisema, mradi huo umegharamiwa na Serikali kuu kupitia Wizara ya Maji na kutekelezwa na Ruwasa Wilaya ya Tunduru kwa kutumia njia ya force Account ambapo pia wananchi wanachangia nguvu zao kwa kushiriki shughuli za ujenzi.

Chanzo: habarileo.co.tz