Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Milioni 976.8/- kugharamia maji Mbinga

D9725c59acf2eab21b5c32105324b690.png Milioni 976.8/- kugharamia maji Mbinga

Mon, 19 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Maji imetenga Sh 976,852,721 kutekeleza miradi miwili ya maji katika kijiji cha Luhagara na Amanimakolo wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Kati ya fedha hizo, Sh 488,197,988 zimetengwa kutekeleza mradi wa Amanimakolo utakaowanufaisha wakazi 3,551 ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 30 na Sh 448,654,733 zimetengwa kutekeleza mradi wa maji Luhagara.

Meneja ufundi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea, Jafari Yahaya alisema mradi wa maji Amanimakolo umeanza kutekelezwa Januari 2020 na unatarajiwa kukamilika Juni mwaka 2021 ambapo Wizara ya Maji tayari imetoa Sh 82,514,784.

Katika mradi huo kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa chanzo cha maji, kuchimba mitaro na kulaza bomba za kusafirisha maji umbali wa km 8.05.

Alitaja kazi nyingine ni kulaza bomba za kusambaza maji kilomita 9.586, kujenga matangi mawili ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 150,000 kwa Kijiji cha Amanimakolo na lita 50,000 Kijiji cha Mkeke pamoja na ujenzi wa vituo 28 vya kuchotea maji.

Hata hivyo alisema kazi zilizofanyika ni ujenzi wa chanzo cha maji, kuchimba mitaro na kulaza bomba za usafirishaji maji kilometa 7.15 na kulaza bomba za kusafirisha maji umbali wa kilometa 0.85.

Kwa upande wa mradi wa Luhagara, Jafari alisema Souwasa ilipokea maagizo kutoka Wizara ya Maji kutekeleza mradi wa maji katika kijiji hicho ambao utekelezaji wake ulianza Januari 2020 na unatarajiwa kukamilika Juni 2021.

Alibainisha gharama za ujenzi wa mradi ni Sh 448,654,733 ambapo Wizara ya Maji imetoa Sh 24,710,921 na mradi huo utawanufaisha zaidi ya wakazi 3,452 pindi utakapokamilika.

Alisema kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa nyumba mbili za kuhifadhi mitambo, ununuzi na ufungaji wa pampu za mfumo wa jua, kuchimba mitaro na kulaza bomba za kusafirisha maji kilometa 1.778.

Alisema kazi nyingine ni kulaza bomba za kusambaza maji kilometa 19.323,kujenga matangi mawili yenye ujazo wa lita 50,000 kila moja na kujenga vituo 30 vya kuchotea maji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz