Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Milioni 560.7 zatekeleza mradi wa maji Wanging'ombe

Milioni 560.7 Zatekeleza Mradi Wa Maji Wanging'ombe Milioni 560.7 zatekeleza mradi wa maji Wanging'ombe

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imetumia Sh.milioni 560,788,295 kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19 kutekeleza mradi mkubwa ya maji katika vijiji vya Igula Halmashauri ya wilaya Wanging’ombe mkoani Njombe.

Fedha hizo zimewezesha kumaliza kabisa kero ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili wakazi 1,780 wa vitongoji vya Azimio, Kidegenge, Kiginga na Mlowa ambao kwa sasa wanapata huduma ya maji safi na salama kwa masaa 24.

Hayo yamesemwa na kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Wanging’ombe Msafiri Tematema,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Waandishi wa habari walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) katika mikoa nyanda za juu kusini.

Tematema alisema, chanzo kikuu cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 10,000 kwa saa ambacho kimefungwa pampu yenye uwezo wa kuvuta maji lita 8,000 kwa saa.

Alisema, kazi ya ujenzi wa mradi imekamilika kwa asilimia 100 na sasa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao, hivyo kuondokana na adha kubwa ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye vyanzo na visima vya asili.

Alieleza kuwa,serikali kupiti wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa) wilaya ya Wanging’ombe na mkoa wa Njombe, imeamua kujenga mradi huo kutokana na upungufu mkubwa wa maji katika kijiji hicho ambacho kinahudumiwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mzingira Wanging’ombe(WANGIWASA).

Aidha alisema, Ruwasa wilaya ya Wanging’ombe imekamilisha mradi mwingine wa maji katika kijiji cha Samaria na kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi 1,873 wa kijiji hicho.

Alisema, mradi huo umetekelezwa kwa njia ya Force Akaunti kwa gharama ya Sh.milioni 380 na zimetumika kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na umekamilika kwa asilimia 100.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Wanging’ombe (WANGIWASA) Mussa Masasi alisema,mamlaka hiyo inatoa huduma ya maji kwa vijiji 54 vilivyopo katika wilaya ya Wanging’ombe kikiwemo kijiji cha Igula.

Alisema, mradi huo umetokana na maombi kutoka kwa uongozi wa serikali ya kijiji cha Igula kutaka kuchimbiwa kisima ili kukabiliana na kero ya huduma ya maji, hata hivyo mamlaka haikuwa na fedha na walipeleka ombi hilo kwa Ruwasa ili iweze kuwasaidia.

Masasi, ameishukuru Ruwasa kutoa kiasi cha Sh. Milioni 560,788,295 ambazo zimefanikisha kukamilika kwa mradi huo na sasa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao.

Alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo,kazi kubwa inayofanyika kwa sasa ni mamlaka kuongeza wateja wengi zaidi ili kupata mapato ambayo yatawezesha kujiendesha,kuboresha huduma na kupanua mtandao kwa lengo la kuwapunguzia wananchi muda wa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.

Pia alisema kuwa, kabla ya kujengwa kwa mradi huo mapato ya mamlaka hayakuzidi shilingi milioni 1 kwa mwezi lakini ni matumaini yake kupitia mradi huo mpya mapato yataongezeka hadi kufika milioni 7 kwa mwezi.

Amewataka wananchi,kuhakikisha wanalinda miundombinu na kutunza miradi inayojengwa, kutumia maji kwa uangalifu na kulipia gharama za maji ili kuijengea uwezo mamlaka hiyo iweze kujiendesha bila kutegemea ruzuku na msaada kutoka serikali kuu.

Mkazi wa kijiji cha Igula Aisha Athuman alisema, shida ya maji katika kijiji hicho ilikuwa kubwa ambapo walilazimika kwenda hadi kijiji jirani cha Ilembula kufuata huduma maji kwa matumizi ya kila siku.

Alisema, ukosefu wa maji safi na salama ulipelekea hata wanafunzi kushindwa kuhudhuria vipindi hasa wakati wa asubuhi kwa kuwa walilazimika kwenda mtoni kutafuta maji kwa ajili ya usafi wa mazingira na matumizi mengine kabla ya kuingia darasani na hivyo kuathirika sana kitaaluma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live