Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mil 20/- kupanda miti Sengerema

6287ba8ae9ebb0a4cf4017e95c0fe6dc.png Mil 20/- kupanda miti Sengerema

Fri, 11 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKALA wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS), unatarajia kutumia Sh milioni 20 katika Mwaka wa Fedha 2020/21 kupanda miti 70,000 wilayani Sengerema.

Ofisa Mhifadhi Msaidizi wa TFS, Newton Mlay, alibainisha hayo juzi wilayani hapa wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Dk Emmanuel Kipore, kwenye tukio la upandaji wa miti 500 katika Shule ya Sekondari Nyamprukano ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika.

Alisema mpango wa TFS kwa Wilaya ya Sengerema ni kusambaza miti 70,000 kwa taasisi za serikali, shule za serikali na za binafsi ili kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi wa wanananchi wa Sengerema na taifa kwa jumla.

Kwa mujibu wa Mlay, upanda miti katika shule hiyo ulilenga kuwaandaa vijana wa kike na kiume kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa miaka ijayo.

Alisema kati ya miti 70,000, TFS tayari imeshapanda miti 11,500 katika wilaya hiyo na kutoa mwito kwa wananchi walio tayari kupanda miti, waende katika ofisi za TFS kuchukua miti kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao.

“Tutahakikisha tunapanda miti kwa taasisi na shule kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na ukuaji wa uchumi,” alisema na kuongeza kuwa, katika mwaka wa fedha ujao, TFS itahamasisha wananchi na taasisi kupanda miti ya matunda.

Akizungumza baada ya kushiriki kupanda miti katika shule hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Dk Kipore aliushukuru uongozi wa TFS kwa kushiriki kikamilifu kwenye utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kila mwaka.

Alisema serikali imeona ni vyema kuitumia maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika kwa kushirikiana na TFS kupanda miti na kwamba kazi hiyo itakuwa endelevu.

Aliutaka uongozi wa Shule ya Sekondari Nyampulukano na wananchi wa Sengerema kuhakikisha wanalinda miti hiyo na kuitunza kwa kuwa ni uhai.

Dk Kipore alisema serikali itawachukulia hatua za kisheria wananchi wanaokata miti hovyona kusisitiza kuwa, ukataji miti lazima uambatane na vibali.

“Ni vizuri tulichukulie jambo hili kwa umuhimu, aidha kupitia hafla hii niwaagize TFS kutoa miti mingine ili kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari apande miti miwili hadi mitatu,” alisema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyampulukano, Christine Zegera, aliishukuru Serikali kwa kuwezesha kupanda miti 600 shuleni hapo na kuahidi kuitunza.

Chanzo: habarileo.co.tz