Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikopo maalumu Sh mil 583.8 yatolewa Uvinza

012216e314c93554978c94cc50ce0f86.jpeg Mikopo maalumu Sh mil 583.8 yatolewa Uvinza

Mon, 13 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumla ya Sh milioni 583.8 zimetolewa mkopo na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013 ikiwa ni uwezeshaji kwa makundi maalumu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya Wilaya Uvinza, Bernad Lusomye alisema hayo akitoa taarifa wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi 20 vya wanawake, vijana na walemavu zenye thamani ya Sh milioni 142 ikiwa ni asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ya halmashauri hiyo.

Lusomye alisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya kuanzishwa kwa halmashauri hiyo imeweza kutoa mikopo kwa vikundi 111 ambapo kati yake vikundi 64 vya wanawake vilipata Sh milioni 313.7 na vikundi vya vijana 39 vilipata Sh milioni 219. Sambamba na hivyo Ofisa maendeleo wa jamii Wilaya ya Uvinza alisema kuwa kwa kipindi hicho halmashauri ilitoa Sh milioni 51 kwa watu wenye ulemavu.

Pamoja na kutolewa kwa mikopo hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Uvinza, Zainabu Mbunda alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya urejeshaji ambapo hadi sasa kati ya Sh milioni 583 zilizokopeshwa ni Sh milioni 258 ndizo zilizorejeshwa.

Akikabidhi hundi kwa vikundi vilivyopitishwa, Mkuu wa Wilaya Uvinza, Hanaf Msabaha amevitaka vikundi vya vijana kubadilika na kuonyesha mfano katika utekelezaji wa fedha za mikopo zinazotolewa na halmashauri kwa kuweza kuendesha shughuli zao kwa tija na kurejesha mikopo.

Msabaha alisema vikundi vya wanawake vimekuwa na mwamko mzuri wa kuomba na kurejesha mikopo na kuwa mfano wa kuigwa na ndiyo maana vikundi vingi vya wanawake vimepata mikopo kutokana na uaminifu wao .

Chanzo: www.tanzaniaweb.live