Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikoa ya Kanda ya Ziwa yang’ara matokeo la saba

Eac5ea5b337a877b6b4ff0f5352d9b91 Mikoa ya Kanda ya Ziwa yang’ara matokeo la saba

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MIKOA ya Kanda ya Ziwa imeng'ara kwenye matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020 kutokana na shule nane kuwa miongoni mwa 10 bora kitaifa, kutoka katika mikoa hiyo.

Aidha, kati ya watahiniwa 10 bora kitaifa, wanane wanatoka mikoa hiyo huku pia katika kundi la wasichana 10 bora kitaifa, saba wanatoka mikoa hiyo na kati ya wavulana 10 bora, wanane wanatoka kwenye mikoa ya Mara, Shinyanga, Simiyu, Kagera na Mwanza.

Akitangaza matokeo hayo juzi jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa(NECTA), Dk Charles Msonde alisema Kanda ya Ziwa imefanya vizuri kwenye matokeo hayo kwa kuongoza kwenye matokeo ya watahiniwa bora wa kike na wa kiume na kundi la shule bora.

Katika shule 10 bora kitaifa, Mkoa wa Kagera unaongoza kwa kutoa shule tatu, ambazo ni Bunazi Green Acres, Kemebos na Rweikiza. Unafuata Mara uliotoa shule ya Twibhoki na Graiyaki na Shinyanga uliotoa shule ya Kwema Modern na Rocken Hill. Mkoa wa Mwanza umetoa shule moja ya Mumtaaz.

Mikoa mingine ambayo si ya kanda ya ziwa iliyotoa shule katika 10 ni Mbeya wenye shule ya God's Bridge na Dar es Salaam ni shule ya St Anne Marie.

Kwa upande wa watahiniwa 10 bora wa kitaifa wa kike, Mara umetoa watahiniwa saba wanaotoka shule ya Twibhoki na Graiyaki, Kagera umetoa wawili kutoka shule ya Rweikiza na mkoa wa Geita umetoa mwanafunzi mmoja kutoka shule ya Samandito.

Katika kundi la watahiniwa bora wa kiume 10, Shinyanga na Mara imeongoza kwa kutoa kila mmoja watahiniwa bora wanne.

Kwa upande wa Mkoa wa Simiyu, umeongeza kiwango cha ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo ambapo shule 10 za mkoa huo ndani ya kipindi hicho zimeonekana kupanda kiwango hicho.

"Kuna mikoa imefanya vizuri kwenye ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo nayo ni Simiyu nafasi ya kwanza, Mara nafasi ya pili na Lindi nafasi ya tatu'',alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz