Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonyesha mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara na Lindi inaongoza kwa idadi kubwa ya wazee wenye umri zaidi ya miaka 65.
Ripoti hiyo ilizinduliwa Zanzibar na Waziri Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Kitaifa, Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, Hemed Suleiman Abdulah Aprili 15, 2023.
Ripoti hiyo, inaonesha Mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kuwa na idadi kubwa ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 65 kwa asilimia 7.3 ambayo ni sawa na wazee 135,921 ikifuatiwa na Mtwara yenye asilimia 6.4 sawa na wazee 104,636.
Aidha, Lindi yenye wakazi milioni 1.2, asilimia sita ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 65 ambayo ni sawa na watu 71,641. Sawa na katika kila watu 10, wastani wa mtu mmoja ni mzee kwenye mikoa hiyo.
Kwa upande wa mikoa yenye idadi ndogo ya wazee, ripoti hiyo inautaja Mkoa wa Katavi kuongoza kwa asilimia 2.3 ukifuatiwa na mikoa ya Dar es Salaam, Mjini Magharibi na Geita yenye asilimia 2.4 kwa kila mmoja.
Hata hivyo, wastani wa kitaifa unaonyesha kati ya Watanzania milioni 61.7, wenye umri zaidi ya miaka 65 ni asilimia 3.8 pekee ambayo ni sawa na watu milioni 2.3.