Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikataba ya uboreshaji barabara, mifereji Temeke yasainiwa

61254 Mkatbapic

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam imesaini mkataba na kampuni tano kwa ajili ya ujenzi wa barabara na mifereji iliyopo kwenye kata mbalimbali za manispaa hiyo itakaogharimu kiasi cha fedha Sh62.4 bilioni.

Akizungumza Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Ludubilo Mwakibibi jana Jumatatu Juni 3, 2019 alisema manispaa hiyo ni miongoni mwa halmashauri zinazotekeleza miradi ya Maendeleo kwa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ambapo mradi huo unatekelezwa kwa fedha za mkopo wa Serikali kutoka Benki ya Dunia (WB).

Alisema wamesaini mkataba na kampuni hizo kwa ajili ya ujenzi wa barabara na mifereji hiyo ambapo inatarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi 15.

Mwakibibi alizitaja kampuni zilizosaini mkataba huo zikiwemo China Railway Seventh Group Co LTD,CRJE(East Afrika)Limited,Jassie &Company LTD na Eristic(T) Investment LTD.

"Miradi ambayo imesainiwa ni ujenzi wa barabara na uboreshaji wa huduma za jamii kata ya Mtoni eneo la Bustani, Sabasaba na Reliini utagharimu Sh18.4 bilioni na Kata ya Mbagara eneo la Kizinga na Baghudad utagharimu Sh12.6 bilioni na ujenzi wa miundombinu ya kudhibiti mafuriko na ujenzi wa mifereji Gerezani Creek utagharimu Sh18.7 bilioni," alisema Mwakibibi.

Ujenzi mwingine wa miundombinu ya kudhibiti mafuriko na ujenzi wa mifereji eneo la mto wa Mzinga utagharimu Sh8.4 bilioni na gharama ya ununuzi wa vifaa vya usafirishaji wa taka utagharimu Sh4.1 bilioni.

Pia Soma

Mwakibibi alisema hadi kufikia Juni 3,2019,manispaa hiyo imepokea Sh210 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na ununuzi wa vifaa vya usafirishaji.

Naye Meya wa Manispaa hiyo, Abdallah Chaurembo alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo wamebakisha barabara moja ya Kilungule ambayo wanaamini wataijenga hivi karibuni.

"Halmashauri hiyo imekuwa ya kwanza kutekeleza miradi ya DMDP na leo hii tumesaini mikataba ya ujenzi yenye thamani ya Sh62.4 bilioni ambapo fedha hizo ni za mkopo wa benki ya Dunia nawasisitiza kulipa kodi ili deni hili liweze kulipwa hivyo watendaji walisimamie suala hili vizuri," alisema Chaurembo

 

Chanzo: mwananchi.co.tz