Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miili ya dereva, tingo yaopolewa ajali ya lori lililolipuka Butiama

Lori Ajali Kahama.png Miili ya dereva, tingo yaopolewa ajali ya lori lililolipuka Butiama

Tue, 5 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Butiama. Miili ya dereva na tingo wake iliyokuwa imenasa kwenye lori lililotumbukia mtoni, kulipuka na kuteketea kwa moto imeopolewa.

Kuopolewa kwa miili hiyo ni matokeo ya kazi na juhudi za saa kadhaa za Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara baada ya kupata mitambo ya kunyanyulia vitu vizito (crane) kutoka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) lililomudu kunyanyua mabaki ya gari hiyo.

Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema tayari mwili wa dereva wa gari hilo lililotumbukia mtoni na kuteketea kwa moto katika tukio lililotokea alfajiri ya leo Jumatatu Desemba 4, 2023, umetambuliwa kuwa ni Michael Dida (30), mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu. Amesema mwili wa mtu mwingine anayeaminika kuwa ni utingo wa lori hilo bado haujatambuliwa.

"Miili yote imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Mara kusubiri taratibu ikiwemo kutambuliwa na kuchukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazishi," amesema Kamanda Magere

Ajali hiyo imetokea katika eneo la Makutano ya Barabara ya Tarime-Musoma-Mwanza wilayani Butiama baada ya dereva kushindwa kulimudu gari iliyoacha njia na kutumbukia mtoni kabla ya kulipuka moto na kuteketea.

Lori hilo lililokuwa linatokea jijini Dar es salaam lilikuwa na shehena la pipa 160 zenye kemikali aina ya Ethanol inayotumika kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji viwandani ikiwemo kutengeneza pombe kali.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amewataka wakazi wa eneo la Makutano kusitisha matumizi ya maji ya Mto Makutano hadi pale wataalam watakapokamilisha uchunguzi na kuthibitisha kuwa hayana madhara kwa binadamu na viumbe hai vingine.

Halfan Yusuf, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo amesema lori hilo lilitumbukia mtoni baada ya dereva kushindwa kuzunguka mzunguko wa njiapanda ya Makutano.

‘’Niliona gari likishindwa kuzunguka mzunguko wa barabara na kutumbukia mtoni kabla ya kutokea mlipuko mkubwa ndani ya sekunde chache. Sikuona mtu yeyote akitoka ndani ya gari lile kwa jinsi mlipuko ulivyotokea na ukubwa wa moto. Hata sisi hatukuthubutu kusogea karibu,’’ amesema Halfan

Chanzo: www.tanzaniaweb.live