Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miili tisa ya waliofariki ajali Njombe yaagwa

Miili Pic Data Majeneza ya Marehemu hao

Tue, 26 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miili tisa ya waumini wa Kanisa Katoliki mkoani Njombe waliofariki kwa ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha Igima wilayani Wanging'ombe Aprili 24, 2022 imeagwa katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Njombe.

Akizungumza wakati wa ibada ya kuaga miili hiyo leo Jumanne Aprili 26, 2022, Mkuu wa Mawasiliano wa Jimbo hilo, Padri Eusebius Kyando amesema Umoja wa Vijana Katoliki Jimbo la Njombe (Uvikanjo) pamoja na walezi wao walipata ajali wakiwa wanarudi katika safari yao ya kitume walikokwenda kuwatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika kituo cha Dorothea Upendo kilichopo Ibumila Parokia ya Mtwango.

Amesema katika ajali hiyo, watu watatu walifariki papo hapo na wengine sita walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu hospitalini.

Amesema toka mwaka 2020 Uvikanjo Parokia ya Njombe wamekuwa wakifanya kazi ya utume kwa kutembelea jumuiya ndogondogo na watu wenye mazingira magumu na kufanya matendo ya huruma katika vituo hivyo.

"Vijana wetu walipata ajali na wengine kufariki wakiwa katika harakati za kitume yaani kueneza injili kwa njia ya matendo mema" amesema Padri Kyando.

Amesema utume huo umewafanya vijana wengi kuimarika katika imani na hofu ya Mungu hasa katika kumpenda Mungu kupitia wahitaji.

Advertisement Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Waziri Kindamba amesema baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo alivielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe na ya Halmashauri ya mji Njombe kwa ajili ya kuangalia majeruhi pamoja na marehemu wa ajali hiyo.

Amesema baada ya kutoka hospitalini akiwa na kamati ya ulinzi ya Mkoa walienda katika eneo ambalo ajali hiyo ilitokea ili kujionea hali halisi.

Amewataka waumini na wananchi wa Mkoa wa Njombe kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

"Kama neno la Mungu linavyosema shukuruni kwa kila jambo kwani hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu" amesema Kindamba.

Amesema Serikali ya Mkoa wa Njombe kama ilivyo kwa kanisa nayo inahitaji nguvu ya vijana kuweza kutekeleza majukumu ya taifa hivyo pigo hilo si la kanisa pekee bali hata kwa Serikali.

"Sisi tuliobaki tujiulize tutaondoka kwa mtindo upi ni vizuri tukajiandaa kwa kunyoosha matendo yetu na tabia zetu ili tutakapoondoka tuondoke vizuri maana kifo ni mawaidha" amesema Kindamba.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbinga anayesimamia Jimbo la Njombe, Askofu John Ndimbo ameishukuru Serikali ya Mkoa huo kwa kushiriki kwa ukaribu tangu tukio hilo litokee.

"Narudia tena kulishukuru Jeshi letu la Polisi kwa kuitika mara moja baada ya kusikia ajali na kufika kutoa miili ya marehemu na majeruhi wetu" alisema askofu Ndimbo.

Baadhi ya waumini walioshiriki ibada hiyo wamesema msiba huo umewagusa kwa kiasi kikubwa na kuwaumiza kwani ni tukio kubwa kutokea hivi karibuni mkoani hapa.

Wametoa wito kwa madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani

Chanzo: www.tanzaniaweb.live