Miili sita kati ya saba ya watu waliofariki jana Jumatano Julai 5, 2023 katika ajali ya Lori kuwagonga watu waliokuwa wakijaribu kumuokoa dereva bodaboda aliyegongwa na gari dogo (IT), imetambuliwa na kuanza kuchukuliwa na ndugu zao, huku majeruhi 10 wakiruhusiwa kutoka hospitali.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa ACP Theopista Mallya amesema kati ya watu hao saba (wote wanaume) waliofariki, sita wameweza kutambuliwa na ndugu zao na miili yao imehifadhiwa katika kituo cha Afya Tunduma.
Amewataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Baraka Mwankenja (25) maarufu kama Fally Ipupa ambaye ni dereva wa bodaboda aliyefariki akitibiwa kituo cha afya, Aizack Kasebele (28), Baraka Lutufyo (23), Fred Karagwe(28), Emmanuel Mlay (24) na John Kapizo (25) wote wakazi wa Tunduma.
Aidha Kamanda Mallya amewataja majeruhi wanaoendelea na matibabu katika kituo hicho cha afya Tunduma kuwa ni Zainab Hassan (43), Oliva Ngusa (38), Hassan Kwambaza (45) ambaye ni dereva wa Lori.
Lori hilo baada ya kugonga kundi hilo la watu pia liliendelea kugonga magari mengine likiwemo gari dogo la abiria (Hiace) lililokuwa na abiria ndani pamoja na bajaji.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Momba ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Farida Mgomi, jana jioni aliwatembelea majeruhi ili kuwajulia hali ambapo amewaambia waandishi wa habari kuwa hali zao zinazidi kuimarika na kwamba majeruhi 10 wameruhusiwa huku wengine wanne wakisubiri kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Mgomi ametoa pole kwa familia za watu waliopoteza ndugu zao na kuwa Mungu awape faraja katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.