Jeshi la Polisi kwa kushirikia na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Arusha limeopoa miili mitano ya watu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Jumatatu Novemba 13, 2023.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Salvas Makweli amesema bado utambuzi wa umri na majina wa miili hiyo iliyoopolewa na Jeshi la Polisi unaendelea kufanyika.
"Hadi sasa tumeopoa miili mitano (saa 8 mchana) akiwamo mwanamke mmoja na wanaume wanne ambao wametambulika kwa majina ya Living Shirima (30), Ally Abdi na Wilson Rajabu wote wakazi wa Jiji la Arusha," amesema.
"Bado uokozi unaendelea katika maeneo mbalimbali tunapoendelea kupata taarifa zaidi tutawajuza,”amesema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Arusha, Osward Manjejele amesema mbali na miili hiyo pia watu sita wameokolewa na wakiwa hai.
"Mbali na hao tumeokoa watu sita usiku saa saba katika maeneo mbalimbali, niwaombe wakazi wa Arusha wachukue tahadhari wenyewe kwa maisha yao hasa wanaoishi mabondeni,"amesema.