Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miili mitano yatambuliwa ajali iliyoua sita Arusha

Ajali Arusha Jana.png Miili mitano yatambuliwa ajali iliyoua sita Arusha

Mon, 18 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miili mitano kati ya sita ya watu waliofariki dunia jana Machi 16, 2024 kwenye ajali iliyohusisha gari ndogo ya abiria (daladala) na lori la magogo aina ya Fiat, iliyotokea katika mji mdogo wa Ngaramtoni, wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, imetambuliwa.

Katika ajali hiyo iliyotokea saa 2:30 usiku, watu watano walifariki dunia papo hapo na wengine 15 kujeruhiwa.

Mtu mmoja bado hajatambuliwa aliyefariki dunia wakati akipatiwa huduma katika Hospitali ya Seliani iliyoko Ngaramtoni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amesema ajali hiyo iliyotokea katika mji mdogo wa Ngaramtoni Barabara ya Namanga - Arusha.

Kamanda Masejo amewataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Evaline Reuben, Linna Massawe, Salmin Amiri, Abutwaiyo Mohamedi na Stella Mushi, wote ni wakazi wa Arusha.

Masejo amesema miili yote mitano ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Seliani na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo hiyo.

“Katika ajali hiyo baadhi ya watu waliojeruhiwa waliruhusiwa baada ya kuonekana hali zao ni nzuri, huku 15 wakilazwa kwa matibabu akiwamo Abiudi Jackson, Hassan Mwanga, Hamidu Mgala, Isack John na Hassan Issa,” amesema.

Kamanda Masejo amesema majeruhi wengine ni Rukia Juma, Sia Mathayo, Paulina Frank, Upendo Michael, Jenifer Richard, wengine ni Regina Marko, Hadija Juma na Julieth Venance, na Vaileth Temba.

“Chanzo halisi cha ajali hiyo hakijafahamika lakini uchunguzi wa awali unaonyesha ni uzembe wa dereva wa lori kupaki njiani, hivyo tunaendelea kumtafuta tukisubiri dereva wa daladala apate nafuu kwani ni mmoja wa majeruhi,” amesema Kamanda Masejo.

Mashuhuda wa tukio hilo, Samweli Kuresoi amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa daladala aliyekuwa amepakia abiria kiasi cha kushindwa kuhimili gari lake baada ya kukutana na lori hilo lililokuwa limepaki.

“Unajua leo Jumamosi ni mnada wa Oldonyosambu na abiria wengi waliokuwa kwenye hilo gari ni wafanyabiashara waliokuwa wanatokea mnadani kurudi makwao, nadhani ndio sababu dereva alikuwa mwendokasi kiasi cha kushindwa kuhimili gari kwani alitaka kuwahi kufika mjini arudie abiria kwa ruti nyingine,” amesema Kuresoi.

Shuhuda mwingine, Samson Martine amesema wakiwa barabarani kusubiri daladala, walipitwa na gari hilo, likiwa na mwendo mkali na mita chache walisikia kishindo kikubwa na baada ya kusogea eneo la tukio walishuhudia waliokuwa abiria ndani wakiwa katika majeraha makubwa.

Mmoja wa majeruhi akizungumza ndani ya wodi katika Hospitali ya Seliani, Hassani Mwanga amesema akiwa katika safari ya kurudi Arusha kutokea Ngaramtoni alisikia kishindo kikubwa na hakuweza kujitambua hadi asubuhi ya March 17, 2024 na kujikuta akipatiwa matibabu.

“Wengi wa abiria tulikuwa tumesinzia kutokana na uchovu wa mchana kutwa na hiyo ilikuwa ni usiku; mimi nilishtuka kusikia kishindo kikubwa na nilipofungua macho niliona watu wametapakaa damu, sikujua tena kilichoendelea hadi leo alfajiri kujikuta niko hospitali nikiwa na maumivu makali sehemu za mbavu, mguu na kifuani,” amesema Mwanga.

Ajali hiyo ni ya pili kutokea ikiwa zimepita siku 22 pekee tangu kutokea ajali nyingine iliyohusisha magari matatu katika mji huohuo wa Ngaramtoni.

Ajali hiyo iliyoua watu 25 na kujeruhi wengine 21, ilitokea Februari 24,2024.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live