Vijana zaidi ya 100 walioshiriki ibada ya maziko ya Nelson Mollel (32), aliyefariki eneo la Sanawari wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, baada ya kupewa adhabu ya kuchapwa viboko kutokana na tuhuma za kumtukana mama yake mzazi, wanaonekana wakisinzia licha ya kuwa ni mchana.
Muda ulivyozidi kwenda ndivyo baadhi ya vijana hao walivyokuwa wakisinzia, wengine wakiwa wameinamisha vichwa huku wakifumba macho na wengine kukoroma kama wameelemewa na usingizi.
Hali waliyokuwa nayo iliwafanya washindwe kumsaidia Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mjini Kati, Daniel Sadera aliyekuwa akiongoza ibada ya maziko kuonyesha kukerwa na hali hiyo na kuamsha baadhi ya vijana waliokuwa wanasinzia karibu yake wakati ibada ikiendelea.
Baada ya mwili wa kijana huyo kuingizwa katika kaburi, vijana waliokuwa katika maziko hayo walionekana wakifukia kaburi hilo kwa mikono, jambo lililofanya zoezi hilo lichukue muda mrefu zaidi.
Mchungaji huyo alihusisha hali hiyo na matumizi ya dawa za kulevya, unywaji wa pombe za kienyeji uliokithiri katika eneo hilo.
“Niombe jamii tuone jinsi ya kuwajibika kwa ajili ya vijana na watoto wetu, wazazi zingatieni maadili, angalia vijana wa miaka 30 hadi 18 hata ukimuambia nyanyua tofali hawezi, kwa ajili ya dawa za kulevya, bangi na sigara au pombe,” alisema Mchungaji Sadera.
“Kina mama wa Kiarusha mnachangia hili kukumbatia watoto, laiti tungechukua wajibu wetu mapema mengi tungeyaepuka kama hili, tuwafundishe watoto maadili ya imani kwa kuwa kuna umri huwezi kumsemesha kama hana maadili ya kijamii au kiimani.
“Misingi tumeiharibu sisi wenyewe, hata haya tunayoona ni madogo na yanatuuma, tujifunze kupitia matukio haya, wazazi tumechangia sehemu kubwa familia na jamii kuharibika kwa sababu ya kutokusimama kwenye haki.”
Kutokana na hali hiyo, kiongozi wa kanisa aliwataka wazazi kuzingatia suala la malezi kwa kuwa ni aibu vijana kuwa katika hali hiyo na kuongeza kuwa baadhi ya wazazi na walezi wanachangia watoto wao kukosa maadili na kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya kwa kukumbatia watoto na kutowafundisha maadili, ikiwemo ya kiimani.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya dawa za kulevya 2021 kutoka Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), mwamko wa kutaka kuachana na uraibu huo umeonekana kwa waraibu 3,109 waliopata huduma hiyo, kati yao 2,949 wakiwa ni wanaume.
Mratibu wa Magonjwa ya Akili Mkoa wa Arusha, Dk Charles Migunga anataja sababu zinazochochea matumizi ya dawa za kulevya kuwa ni pamoja na makundi mabaya ya kijamii, kushindwa kujitambua (stadi za maisha) miongoni mwa vijana, migogoro na utengano wa familia.
Tanzania imeendelea kushuhudia wimbi la vijana kuingia bila kujua katika vihatarishi vya dawa za kulevya, huku Serikali ikiendelea kupambana na dawa hizo nchini, ikiwamo kuongeza idadi ya nyumba za upataji unafuu (sober houses) kwa waraibu wa dawa hizo kutoka nyumba 33 mwaka 2020 hadi kufikia 44 mwaka 2022.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utoaji wa huduma ya tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya katika vitengo vya afya ya akili vilivyopo sehemu mbalimbali hapa nchini waraibu 891,117 kati yao wanaume wakiwa 454,390 na wanawake 436,727 wanapatiwa huduma hiyo kwenye hospitali hizo, huku idadi kubwa wakionekana kuathirika na matumizi ya vilevi kama pombe, bangi, mirungi, heroin na cocaine.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya dawa za kulevya 2021 kutoka Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), mkoa wa Arusha kwa mwaka 2020 waraibu waliopata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili walikuwa 12,716, kati yao wanaume wakiwa 10,057 na wanawake 2,659, huku mwaka 2021 idadi hiyo ikiongezeka na kufikia 30,310, kati ya hao wanaume wakiwa 18,970 na wanawake 11,340.
Jacob Yona (38), mkazi wa Moshono jijini Arusha ni mmoja wa vijana walioweza kuacha matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin baada ya kutunzwa na kupatiwa huduma kwa kupitia hatua 12 za upataji nafuu na huduma za unasihi bila kutumia dawa kutoka sober house iliyopo jijini hapa.
“Nilianza kutumia dawa za kulevya mwaka 2005 ikiwa ni miaka miwili tangu nimalize kidato cha nne. Nilivyokuwa sekondari nilianza kutumia bangi na pombe kidogo ila nakumbuka siku moja nilikutana na mtu ambaye hakuwa mwanafunzi akiwa anavuta unga, akanipa nikajaribu ila sikuvuta tena,” anasema.
Anasema baada ya kumaliza masomo aliendelea kuvuta bangi huku akiuza katika eneo la Kijenge Juu, mwanzo aliona ni sawa kwa kuwa hakupata tatizo lolote, ndipo akajikuta amejiingiza kwenye matumizi ya heroin.
“Nimetumia unga kwa kipindi cha miaka mitano ila miaka kama miwili ya mwanzoni nilikuwa sawa, hakuna rafiki au mwanafamilia aliyejua natumia, nilikuwa na mwonekano msafi, nafanya shughuli zangu bila shida.
“Baada ya kuendelea kwa muda nikaanza kujiona mabadiliko, nikapoteza hamu ya kula, usafi niliokuwa nao ukaisha, na nyumani wakagundua ninatumia dawa za kulevya,” anasema.
“Nimefanya matukio mengi magumu ila mojawapo ambalo sitalisahau na lilisababisha nijione sikuwa mtu wa kawaida nilikuwa kama mnyama ni pale kaka yangu alipofariki dunia.
“Nilipopigiwa simu kujulishwa juu ya hilo nikaenda hadi Mt. Meru ila sikuingia mochwari kwanza, nikapitiliza hadi Sanawari nikaenda nikavuta unga ndipo nikarudi pale.
“Nilivyorudi mochwari nikamuona ndugu yangu lakini cha ajabu, alikuwa na vitu vyake kama koti, simu, viatu na nguo nyingine ambapo kitu cha kwanza nilivichukua vyote nikaenda kuuza ili nipate hela ya kununua dawa, tukio hilo linanisikitisha hadi leo,” anasema.
Anasema mwishoni mwa mwaka 2016 aliweza kuacha kutumia dawa hizo za kulevya baada ya kusaidiwa na rafiki yake kupelekwa sober house, hadi sasa ana miaka saba hajatumia dawa hizo.