Migogoro inayotokana na kudhulumiwa viwanja na mashamba ndio yameonekana kutawala katika orodha ya malalamiko ya wananchi yanayopokelewa na wajumbe wa kamati maalum ya kushughulikia kero na matatizo ya wananchi iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla.
Akizungumza leo Oktoba 11, 2023 wakati wajumbe wa kamati hiyo wakipokea na kutatua kero za wananchi wilayani Sengerema, Kiongozi wa Kamati hiyo, Happiness Mtutwa amesema kati ya malalamiko 100 yanayowalishwa mbele ya kamati, zaidi ya nusu inahusu migogoro ya ardhi inayotokana na ama utapeli au kudhulumiana.
Amesema pamoja na kutafuta ufumbuzi wa haraka wa migogoro hiyo, kamati hiyo pia hutoa ushauri kwa wananchi namna ya kuepuka migogoro hiyo.
‘’Moja ya ushauri tunayowapa wananchi ni kujiridhisha na uhalali na umiliki wa ardhi au kiwanja kabla ya kusaini mikataba ya manunuzi ili kuepuka migogoro,’’ amesema Mtutwa ambaye pia ni Kamishina wa Aridhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza
Ametumia fursa hiyo pia kuwaagiza Maofisa Ardhi katika halmashauri za Mkoa wa Mwanza kwenda vijijini na mitaani kuwasikiliza wananchi na kuwapa ushauri namna ya kuepuka migogoro ya ardhi.
Maria Ngeleja, mkazi wa eneo la Bukala Wilya ya Sengerema amesema licha ya matapeli wa mitaani, baadhi ya migogoro ya ardhi inachangiwa na watumishi wa idara ya ardhi wasio waaminifu wanaowezesha utoaji wa hati zaidi ya moja kwa kiwanja kimoja.
Kauli hiyo imeungwa mkono na John Sule akiiomba Serikali kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria watumishi wa idara ya ardhi wanaochangia migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Ofisa Ardhi Mteule Wilaya ya Sengerema, Seth Langwa amesema baadhi ya migogoro ya aridhi ambayo ofisi yake inahangaika nayo muda huu ilitokea miaka kadhaa na ilichangiwa na wahusika kuanzia wauzaji na wanunuzi kutozingatia sheria.