Dar es Salaam. Katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki limeonekana kuzingatiwa vyema na wakazi wa Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Leo Jumamosi Juni Mosi, 2019 Mwananchi limezunguka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo hasa yenye wafanyabiashara wengi na kutoshuhudia mifuko ya plastiki.
Hata waliokuwa wakifika kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kujipatia mahitaji mbalimbali walionekana wakiwa na mifuko mbadala.
Katika masoko ya Tandika na Stereo, wanawake wengi walionekana wakiwa wamebeba vikapu kwa ajili ya kuwekea mahitaji yao.
Mkazi wa Mtoni, Rehema Mbiku ameeleza kuwa katazo hilo limewarudisha wanawake nyakati za kubeba vikapu wanapokwenda sokoni.
“Kwa kiasi fulani linaturudisha enzi za mwanamke wa Kitanzania kwenda sokoni na kikapu binafsi naona Serikali imefanya kitu kizuri mifuko ilikuwa inachafua mazingira,” amesema Mbiku.
Pia Soma
- Walichokisema wafanyabiashara wadogo Dar matumizi mifuko mbadala
- Kishindo cha kumalizika kwa tamthilia ya Sultan