Hai. Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imetoa mifuko 200 ya saruji na tani moja ya nondo kwa lengo la kufanya upanuzi wa kituo cha polisi cha wilaya hiyo.
Leo Alhamisi Mei 23, 2019 mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amemkabidhi msaada huo mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, Lwelwe Mpina.
Sabaya amesema lengo la msaada huo ni kuboresha huduma kwa wananchi katika mji huo, ambao pia ni maarufu kwa shughuli za kitalii.
“Tuna imani saruji hii na nondo vitafanya kazi iliyokusudiwa sitegemei kupata taarifa za kuibiwa hata mfuko mmoja wa saruji hapa, kwani ni eneo salama lenye ulinzi,” amesema.
Amesema kamati yake imejipanga kuhakikisha ndani ya miezi mitatu, jengo jipya la polisi wa wilaya hiyo liwe limekamilika ili wananchi wapate huduma nzuri.
“ili kufanikisha ujenzi mimi mwenyewe nimejiteua kuwa mwenyekiti wa kamati na ndani ya miezi mitatu jengo liwe tayari,” amesema mkuu huyo wa Wilaya.
Pia Soma
- VIDEO: Ndugai, mbunge Masele watuhumiana bungeni
- Mwanamke aua jambazi kwa kisu
- Zao la utomvu laiingizia Saohill Sh700 milioni
- VIDEO: Bunge la Tanzania lamsamehe Masele
Amebainisha kuwa jengo jipya la kituo kikuu cha polisi cha wilaya hiyo litasaidia kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma bora kwa wananchi.
Anna Njau mkazi wa Hai amesema ujenzi wa jengo jipya la polisi utasaidia kupunguza msongamano kiatika kituo hicho kilichopo barabara kuu ya Arusha - Moshi.