Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mifugo kuondoa umasikini

3fe21094f2bcb7950aa2f903f71ec0b0 Mifugo kuondoa umasikini

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imesema itahakikisha sekta za mifugo na uvuvi, zinawaondoa wananchi katika umasikini, kupata ajira na nchi iweze kuuza bidhaa bora za mazao ya mifugo na uvuvi ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jana katika ziara yake mkoani Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba amesema wizara imekuwa ikichukulia kwa uzito mkubwa suala la viwanda, ambalo litaweza kubadilisha fikra za wafugaji na wavuvi.

“Wananchi wetu waondoe umasikini, wananchi wetu wapate ajira na sisi tuuze bidhaa za mazao haya ya mifugo na uvuvi yaliyo bora hapa ndani na kule kwa wenzetu nje, sasa mimi nikikuta hali ya mkwamo kwa kitu ambacho kinatusaidia kuelekea huko napata shida,”alisema Ndaki

Alisema haridhishwi na baadhi ya changamoto wanazokutana nazo wawekezaji, ambao wamejikita katika kuyaongezea thamani mazao ya mifugo na uvuvi.

Alimuagiza Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama nchini, Iman Sichalwe kumpatia taarifa ya hali ya viwanda vya nyama nchini ili apate tathmini halisi ya utendaji kazi wa viwanda hivyo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Chobo, John Chobo alisema kwa sasa kiwanda chake kimesimamisha uzalishaji na kinatarajia kuanza tena uzalishaji mwezi Januari mwakani.

Alisema kiwanda hicho kimekuwa kikisambaza nyama katika nchi za Falme za Kiarabu, lakini ugonjwa wa corona umeathiri biashara katika mataifa mbalimbali duniani.

Pia alisema kutopatikana kwa taarifa sahihi za mifugo, kumechangia kwa kiasi kikubwa soko la nyama kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi kuwekwa katika daraja la chini. Hali hiyo inatokana na mifugo mingi ambayo inachakatwa viwandani, haina taarifa sahihi juu ya ukuaji wake, magonjwa na chanjo mbalimbali ambazo mifugo hiyo imepatiwa.

Kufuatia hali hiyo Waziri Ndaki alisema wizara yake itahakikisha inafuatilia changamoto zinazoihusu wizara hiyo ili kuzipatia majibu.

Chanzo: habarileo.co.tz