Mifugo 345 ikiwemo ng'ombe na mbuzi imekamatwa ikichungwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kinyume cha sheria.
Mbali na mifugo hiyo, askari wa kikosi cha doria wamefanikiwa kuwakamata baadhi ya wakulima waliovamia maeneo ya hifadhi hiyo kwa kulima na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni kati ya maeneo ambao yamekuwa yakiharibiwa na kusababisha madhara ya kimazingira ikiwamo Mto Ruaha Mkuu kukauka.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Kamanda wa Hifadhi ya Taifa Ruaha, Godwell Ole Meing’ataki amesema wanaendelea kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira hususan katika bonde la oevu la Usangu ambapo kuna vyanzo muhimu vya maji kwa ajili ya mto Ruaha Mkuu na bioanuai muhimu kwa mazingira, uhifadhi na utalii.
"Doria inaendelea kufanyika kwa miguu, magari na anga ili kuthibiti wavamizi katika eneo oevu la Usangu wakati wa mchana na usiku," amesema Ole Meing'ataki na kuongeza;
"Tumebaini kuwepo kwa baadhi ya wafugaji ambao wanaendelea kukiuka kwa makusudi maelekezo ya Serikali na sheria za hifadhi kwa kuingiza mifugo hifadhini, kubuni mbinu ya kuingiza mifugo hifadhini wakati wa usiku na kuiondoa mapema sana asubuhi," amesema.
Amesema doria hiyo imefanywa ya Novemba 13 na 14, 2013 kutokana na kukaidi huko na kwamba jambo hilo tayari limefikishwa kwenye vyombo ya sheria kwa hatua zaidi.
Ameongeza kuwa pia ndani ya hifadhi hiyo wamefanikiwa kukamata trekta moja ambayo inashikiliwa wakati taratibu za kulifikisha katika vyombo vya sheria zinaendelea.
"Tunatoa wito kwa wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla kutii sheria, kanuni na kuzingatia maelekezo ya Serikali juu ya kuheshimu na kuzingatia sheria za hifadhi na kutoingia hifadhini au kuingiza mifugo hifadhini na hata kuingia hifadhini kwa ajili ya shughuli ya uvuvi haramu," amesema.
Ameeleza kuwa yeyote atakayekiuka sheria za uhifadhi ajue kwamba atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, amesema vikosi vya doria katika hifadhi na ofisi ya Naibu Kamishna Kanda ya Kusini wapo kazini muda wote tayari kukabiliana na wahalifu wote wanaokiuka sheria na kanuni za hifadhi.