Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mifugo 12,000 katika vijiji sita kufaidi josho

E88220b71fdc0385e7a1f2e4684ef3eb.jpeg Mifugo 12,000 katika vijiji sita kufaidi josho

Tue, 19 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAKRIBANI mifugo 12,000 katika vijiji sita vya kata za Songe na Masagalu imetoka katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mifugo baada ya serikali wilayani Kilindi kukamilisha ujenzi wa josho la mifugo lililokuwa limetelekezwa kwa zaidi ya miaka kumi.

Wakizungumza baada ya uzinduzi wa josho hilo lililojengwa katika kijiji cha Kwamba katika Kata ya Songe, wananchi wa vijiji hivyo ambao wengi ni jamii wafugaji walishukuru wakisema kukamilika kwa ujenzi wa josho hilo kutawondolea kero.

Mmoja wa wafugaji wa jamii ya Kimaasai, Lengisho Shami, alisema wamefarijika kukamilika kwa josho hilo kwani asilimia kubwa ya mifugo ilikuwa ikipoteza maisha kutokana na magonjwa mbalimbali ya mifugo.

Shami alisema kukosa huduma ya josho ilikuwa tishio kwa mifugo yao kutokana na magonjwa.

Issa Nurdin alisema kufunguliwa kwa josho hilo ni fursa kwao kuendeleza sekta ya mifugo kwa kuwa ni moja ya vyanzo vyao vikuu vya mapato.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kwamba lilipo josho hilo, Abdi Makinda, alisema mradi huo ulianzishwa baada ya serikali kusikia kilio chao, lakini kwa zaidi ya miaka kumi ulikuwa umetelekezwa.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kunavinufaisha vijiji sita vilivyopo katika kata za Songe na Masagalu na kwamba, takriban mifugo 12,000 watapata huduma katika josho hilo mara tatu kwa wiki.

Kwa mujibu wa Makinda, vijiji vinavyonufaika na mradi huo ni Kwamba, Miluzi, Kigunga, Misheni, Mheza na Sambu.

Kabla ya kukamilika kwa josho hilo, wafugaji hao walikuwa wakilazimika kufuata huduma hizo Songe umbali iliokuwa na athari kwa mifugo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Gracian Makota, alisema mradi huo umegharimu Sh milioni 37.4.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imechangia Sh milioni 1.16 huku nguvu za wananchi zikiwa ni Sh 300,000.

Chanzo: habarileo.co.tz