Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miezi saba ya gerezani ilivyombadili Simwanza

51621 Gereza+pic

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wengi wanaamini gerezani ni mahala pasipofaa na hakuna kitu chema ambacho mtu anaweza kukipata huko zaidi ya mateso na kukata tamaa.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa gereza ni sehemu ya kumfanya mtu aliyekosea kujutia makosa yake na kubadilika kuwa raia mwema pindi anaporejea kwenye jamii baada ya kumaliza kifungo chake.

Pamoja na kumfanya mtu kuwa raia mwema, gereza linaweza kuwa chuo cha mafunzo hasa ikiwa mfungwa atapokea kwa mwitikio chanya shughuli au kazi anazopewa kufanya kama adhabu akiwa kifungoni.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa kijana Amos Simwanza ambaye anaendesha maisha yake kwa kutegemea biashara ya kuuza uji.

Umahiri wa kupika uji wa mchele anasema aliupata katika Gereza la Segerea alipokuwa amekaa kama mahabusu kwa muda wa miezi saba, kufuatia kesi ya upotevu wa pikipiki.

“Mwaka 2014 niliwekwa mahabusu katika Gereza la Segerea nikiwa kule nikawa napewa kazi za jikoni. Nikakutana na watu wanaojua kupika na ndipo nilipoanza kujua kumbe kuna uji wa mchele,

“Nikamuuliza mzee aliyekuwa akiandaa kama anaweza kunifundisha, hakuwa na hiyana. Huo ukawa mwanzo wa mimi kujua kupika uji lakini sikufikiria kwamba ningekuja kufanya biashara hii,” anasema

Kwa Simwanza kwenda kwake gerezani kumekuwa na faida, kwani ametoka na ujuzi ambao hakuwa nao hapo kabla na sasa ndio anaoutumia kuendesha maisha yake.

Ukibahatika kukutana na kijana huyu ni ngumu kuamini kuwa anachokifanya, hii inatokana na umaridadi na ucheshi alionao kama wale vijana wa mjini wajiitao watanashati..

Muonekano huo haujamfanya awe mwenye kubweteka kwa kukaa vijiweni, muda wake mwingi anatumia kwenye biashara yake na anasifika zaidi kwa umahiri wa kupika uji wenye ladha ya aina yake unaonogeshwa na viungo mbalimbali.

Katika mitaa ya Bagamoyo, Simwanza anafahamika zaidi kama ‘rasta muuza uji’, jina hilo amepachikwa kutokana na mtindo wa nywele alionao kichwani pamoja na biashara yake hiyo.

Kwa Simwanza hilo halina shida kwake ili mradi anapata fedha zinazomuwezesha kumudu maisha yake na hadi sasa anaamini uji ndio mkombozi wake.

“Nakutana na watu wananicheka, wananishangaa inakuwaje mwanaume nafanya mambo ya jikoni kwa madai hizo ni shughuli za wanawake na kila aina ya kebehi

“Kuna wakati nakata tamaa natamani niache hii kazi lakini kila nikifikiria nilikotoka na hapa nilipo naona sina sababu ya kuacha zaidi ya kuongeza bidii ili siku moja watu waniheshimu na waje kujifunza kwangu,” anasema.

Ratiba yake kwa siku

Ili aweze kuwafikia wateja wake mapema, inamlazimu kila siku kuamka saa 11 alfajiri kwa ajili ya kupika uji na kuuhifadhi kwenye chupa tayari kwa kuanza siku mpya.

Inapofika saa 12 anaingia barabarani akiwa na baiskeli aliyoitengeneza kwa mtindo unaomuwezesha kubeba chupa kubwa zisizopungua tano pamoja na vikombe kwa ajili ya wateja wake.

“Mara nyingi maandalizi ya unga kwa ajili ya uji wa kesho nafanya mchana kwani asubuhi na jioni huwa naingia mtaani kusaka wateja.

“Ninapoamka napika uji wa asubuhi naenda kuuza narudi nyumbani kwenye saa nne au saa tano naandaa unga wa kesho nikimaliza saa 10 jioni naingia tena mitaani hadi saa tatu hadi saa nne usiku kwa ajili ya kupumzika,” anasema.

Katika kunogesha biashara yake na kuwavuta wateja wengi hakuishia kwenye uji wa mchele pekee alijifunza pia kupika uji wa ulezi ambao nao anauza.

Iwe sokoni, kwenye vijiwe vya boda boda, ufukweni na popote kwenye mkusanyiko wa watu maeneo ya Bagamoyo mjini kijana huyu anaingia na baiskeli yake kutafuta wateja

Kwa siku Amos anauza chupa kubwa 10 hadi 12 za uji ambazo zinaingia vikombe tisa kwa kila chupa kiwango kinachomuwezesha kuingiza wastani wa Sh45, 000 hadi 50,000 kwa siku.

Nini kilimsukuma kwenye biashara hiyo?

Anasema alianza biashara hii baada ya kutoka gerezani akiwa na umri wa miaka 20 baada ya baba yake kukataa kumlipia ada ili asomee masuala ya sanaa.

“Nilijiunga na chuo cha sanaa cha Tasuba lakini baba akakataa kunilipia ada kwa vile alikuwa hataki nijihusishe na masuala ya sanaa, na mimi sikutaka kusoma kitu kingine kwa kuwa mapenzi yangu yalikuwa kwenye sanaa,

“Nikaona nitafute njia ya kujipatia kipato na wazo la haraka nililofikiria ni kufanya biashara ya uji wa mchele kwa kuwa nilikuwa nafahamu jinsi ya kuandaa baada ya kujifunza gerezani,”

Anasema baada ya kupata wazo hilo changamoto kwake ikawa ni mtaji na namna ya kuanza biashara hiyo, akapata ujasiri wa kuzungumza na jirani yake ambaye alimtia moyo na kumpatia vifaa vya kuanzia na ndipo alipojitosa kwenye biashara kama majaribio.

Uthubutu huo ulizaa matunda kwani kupitia biashara hiyo aliweza kukusanya fedha kidogo kidogo ambazo zilimuwezesha kuanza kujilipia ada.

Aliendelea mtindo huo na hatimaye akafanikiwa kumaliza masomo yake katika ngazi ya cheti kwenye fani ya uigizaji, uchezaji na sanaa za maonyesho.

Pamoja na kupata elimu hiyo mawazo ya Amos bado yapo kwenye uji na anatamani kupata wigo wa kutanua zaidi biashara yake hiyo ili awafikie watu wengi zaidi.

“Nilianza kwa kutembeza kwa miguu sasa nina baiskeli, lakini natamani niweze kupata hata gari ndogo ya wazi ili niweze kusambaza umbali mrefu zaidi,’’ anasema na kuongeza:

“Binafsi nafanya jitihada na hivi karibuni nitafungua mgahawa utakaokuwa na aina mbalimbali za uji, maziwa na vitafunwa lakini bado nitaendelea kuzunguka na baiskeli kuwafuata wateja wangu katika maeneo yao ila kama kuna mtu ataguswa kunisaidia nitafurahi nikipata gari kama vile kirikuu.

Anatamani sana jamii ielewe na kumheshimu kwa kazi yake, kwani anaamini kuwa kwenye utafutaji wa riziki hakuna kazi inayomhusu mwanaume wala mwanamke pekee.

Wito wake kwa vijana ni kutochagua kazi au kuhofia kujishughulisha na kitu kwa hofu ya kuonekana unafanya mambo tofauti.

“Dharau, kebehi na maneno yasiyofaa hayapaswi kukurudisha nyuma kijana au kukukatisha tamaa; fanya chochote ambacho unaona kinaweza kukusaidia ili mradi kiwe halali, anasema akiwapa wosia vijana wenzake wa kiume wanaochagua kazi au kuchelea kufanya kazi zinazoonekana ni za wanawake. Hali ya maisha imekuwa ngumu ukisema ukae usubiri kuajiriwa ofisini unaweza kuishia kuwa mzigo nyumbani, Rais ameshasema hapa kazi hivyo hatuna budi kuchakarika na kufanya kazi ili kujipatia riziki,” anasema.



Chanzo: mwananchi.co.tz