“Wazazi wangu ni wazee kiumri na wamechoka si watu wa kufanya kazi, lakini kwa kuwa sina uwezo tena wa kufanya kazi wanalazimika kutafuta riziki ili tupate chakula na mahitaji mengine ya msingi.”
Ndivyo Marita Malambi (25) anavyoanza kusimulia kuhusu masaibu ya maisha yake baada ya kunusurika kutafunwa na mamba Februari 17, mwaka huu, wakati akichota maji katika Mto Mgeta huko Dakawa, Morogoro, ikiwa ni madhara yatokanayo na kukosekana huduma hiyo muhimu katika kijiji anachoishi.
Marita aliyezaliwa na kukulia kijijini Dakawa Ukutu, wilayani Morogoro Vijijini, anasema kwa sasa maisha yamekuwa na changamoto kwake kiasi hajui hatima yake na familia.
“Kwa sasa nipo tu nyumbani nasubiri wazazi wahangaike ndipo waje wanunue chochote hapa nyumbani ili mkono uende kinywani. Nyumbani naishi mimi, baba na mama pekee,” anasema.
Marita anayeishi kwenye makazi duni kwa kutegemea vyumba viwili pekee vya kulala na yeye kulazimika kulala jikoni, anasema baada ya ajali ya mamba mtoto wake wa miaka mitano alichukuliwa na baba yake, hivyo yeye kubaki na wazazi pekee.
Marita ambaye alirudi kijijini hapo Juni mwaka huu baada ya kutibiwa kwa muda mrefu katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi) akiuguza mguu wake uliovunjwa na mamba huyo, anasema tangu amerejea kijijini hapo hajakanyaga katika mto huo.
“Sijaenda kabisa mtoni na siwezi kwenda kwa mara nyingine. Nahisi mamba bado wapo kwa kuwa huku kwetu hata maji yakipungua kunakuwa na giza, hivyo hata mamba anapokuja huwezi kumuona,” anasema.
Marita anasema kwamba kwa sasa kijijini hapo wamepatiwa visima 13, lakini kwa kuwa yeye na wazazi wake wamejenga mashambani wanalazimika kuteka maji katika kisima kidogo kwenye chemichemi.
“Mashamba yetu yapo ng’ambo na ili kuyafikia lazima uvuke Mto Mgeta. Mimi siwezi kurudi tena huko. Ninachotamani kwa sasa ni kupata chochote ili nifanye shughuli zangu kama kawaida hata biashara.” anasema.
Hali yake kiafya
Marita anasema madaktari walimuwekea chuma pajani.Hawajaniambia watakitoa lini,” anasema huku akifafanua kuwa kutokana na uwepo wa chuma hicho imembidi kuwa mwangalifu na shughuli anazozifanya.
Anasema tangu aanze matibabu baada ya tukio hilo amekuwa akihudhuria kliniki mara kwa mara na madaktari kumshauri mambo mbalimbali juu ya afya yake.
“Mara ya mwisho nilikwenda Agosti 31, mwaka huu, natakiwa kurudi Novemba hii. Ninapokwenda nalipia Sh8,000 za kumuona daktari zaidi ya hapo hakuna kingine ninacholipia. Nilipokwenda hospitali mara ya mwisho niliambiwa mguu unaendelea vizuri hivyo naweza kuendelea na shughuli zangu kama kawaida,” anasema. Hata hivyo, anasema bado anapata maumivu hasa wakati wa baridi kali.
Apokea msaada
Novemba 8, mwaka huu, Marita alipokea Sh349,400 zilizochangwa na wasomaji wa gazeti la Mwananchi ili kumuwezesha kimaisha.
Marita anashukuru kwa msaada huo na kuahidi kuzizalisha kwa kufanya biashara ili zimsadie kiuchumi yeye na familia yake.
“Nalishukuru sana gazeti la Mwananchi na wasomaji wake, Mungu awabariki. Kutokana na matatizo niliyoyapata nisingeweza kufanya kitu chochote, lakini nashukuru leo nimepata fedha hizi nitaweza kuanzisha mradi ili uniwezeshe katika maisha yangu,” anasema Marita.
Anasema hali aliyonayo sasa ni ngumu kuliko awali, hawezi tena kufanya vibarua kama zamani na hata shughuli za mtoni za kilimo cha mbogamboga amelazimika kuziacha kuhofia maisha yake.
Licha ya kuwa Marita anatoka katika kaya masikini, kijiji chao hakijafanikiwa kuingia kwenye mpango wa ruzuku kwa kaya masikini zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Mama wa Marita, Emma Lolensi anasema hajawahi kusikia kuhusu huduma za wasiojiweza kijijini hapo ingawa anasikia wenzao wa vijiji jirani wapo kwenye mpango wa ruzuku inayotolewa na Tasaf.
“Hapa kijijini hakuna vikundi wala msaada wowote. Kuhusu hiyo ruzuku kwa kaya zisizojiweza tumesikia tu kwa wenzetu vijiji vya jirani kama Kisaki kwamba kaya zisizo na uwezo zinapewa msaada kifedha,” anasema Emma.
Mkulima wa kijiji hicho Daudi Alphonce (69), anasema ingawa alifiwa na mkewe na maisha yake ni ya shida, hajafanikiwa kufikiwa na mpango huo bali husaidiwa na baadhi ya ndugu.
“Watoto wangu wawili walifariki amebaki mmoja wa kike ambaye maisha yake pia ni duni, sina msaada wowote. Tunasikia kuhusu hiyo Tasaf lakini haijatufikia hapa kijijini,” anasema.
Mwenyekiti Kijiji cha Dakawa Ukutu, Hassan Mwanga anasema Tasaf iliwafikia awamu ya kwanza, wakajenga madarasa matatu, ofisi moja, lakini mpango wa kusaidia kaya masikini haujawafikia.
Kijiji hicho ambacho kwa miaka mingi kilitegemea maji ya Mto Mgeta wenye mamba wengi, kimepatiwa visima 13.
Visima hivyo vimechimbwa ikiwa ni miezi kadhaa tangu Mwananchi kuripoti habari mfululizo kuhusu uhaba wa maji kijijini hapo Machi mwaka huu.
Mwanga anasema, “Visima hivi vimechimbwa na Taasisi ya Islamic Foundation. Walipanga kutuchimbia 28, lakini wametupatia 13 vilivyochimbwa Septemba.’’
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Duthumi, Dk Kazimili Subi anasema wamekuwa wakipokea majeruhi walioshambuliwa na mamba na kuwatibu.
Anasema wagonjwa walioshambuliwa na mamba na kutibiwa anasema. “Mwaka 2016 tulikuwa na kesi 23 za majeruhi wa mamba miongoni mwao watu wazima na watoto. Mwaka 2017 zilipungua na kuwa 13 na kwa mwaka huu hadi sasa kumeripotiwa matukio matatu kwa kuwa mvua zilichelewa, zikianza kukolea tunaweza kulaza majeruhi hata wawili au watatu,” anasema Dk Subi.
Tukio la kushambuliwa
Marita alishambuliwa na mamba jioni ya Februari 17, 2018 tukio lililosababisha kumpoteza mtoto wake wa kiume, Godfrey David (mwaka mmoja na miezi miwili) aliyekufa na baadaye maiti yake kusombwa na maji.
Baada ya kupambana na mamba kwa muda, alifanikiwa kuokolewa na vijana waliokuwa karibu na mto na kupelekwa Kituo cha Afya Duthumi kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Morogoro, ambako alihudumiwa kwa siku tano na kabla ya kuhamishiwa kwenda Muhimbili na kufanyiwa upasuaji Moi.
Kabla ya upasuaji huo madaktari walifanya jitihada kubwa ya kusafisha vidonda (Surgical debridement) na kumpatia dawa (Antibiotics) ili kuondoa bacteria na kuepusha madhara.