Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Michezo ya kubeti yahatarisha ndoa kuvunjika Ikungi

Michezo Ya Kubeti Yahatarisha Ndoa Kuvunjika Ikungi Michezo ya kubeti yahatarisha ndoa kuvunjika Ikungi

Wed, 24 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ongezeko kubwa la vijana kushiriki michezo ya kubashiri (Kubeti), limedaiwa kusababisha ndoa kuvunjika na kukithiri kwa uhalifu katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Mtunduru, Ramadhan Mpaki wakati akichangia kwenye kamati ya fedha na uchumi katika kikao cha baraza la madiwani cha robo tatu kuanzia Januari hadi Machi 2023 kilichoketi May 19, 2023 wilayani humo.

Mpaki alisema kwa siku za karibuni kumekuwa na kasi kubwa ya ndoa kuvunjika na uhalifu kuongezeka na sababu kubwa ni kutokana na vijana kujihusisha na michezo ya kubashiri.

Diwani huyo alisema iwapo hakutakuwa na hatua za haraka kudhibiti michezo ya kubashiri ni wazi kuwa hali itazidi kuwa mbaya, kwa ndoa kuvunjika na uhalifu kuongezeka.

Mpaki alitoa ushauri kwa baraza la madiwani kuangalia namna ambayo inaweza kufikisha jambo hili katika mamlaka za kutunga sheria ili ziweze kuona namna ya kulitatua, kwani hali ni mbaya kwa sasa hasa kwa wanandoa.

“Naomba halmashauri yetu iangalie upya sheria ya mchezo huu wa kubashiri, kwani pamoja na kuwa chanzo cha mapato vijana wamekuwa wakicheza mchezo huo hadi usiku wa manane ambapo pia wamekuwa wakipanga vitendo vya kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na kutishia ndoa za watu,” alisema Mpaki bila ya kufafanua.

Aidha diwani huyo aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukasanyaji wa mapato, huku wakizingatia misingi ya utawala bora.

Naye Diwani wa Kata ya Mwaru, Iddi Makangale alimpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ally Mwanga na Mkurugenzi, Justice Kijazi kwa mafanikio makubwa inayopata wilaya hiyo chini ya uongozi wao kwa kushirikiana vizuri na watendaji wa kata, tarafa na wataalam.

Pia Makangale alizipongeza kata za Mgungila, Mwaru na Mkiwa kwa kuongoza kwa kukusanya mapato na kuzitaka kata zingine kuiga mfano huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ally Mwanga aliwataka watumishi wote na viongozi kuwa wazalendo na kushirikiana ili kuiletea maendeleo wilaya hiyo.

Mwanga alisema suala la ukusanyaji wa mapato ni la kufa na kupona na akasisitiza uzalendo katika jambo hilo na kuwa uhai wa halmashauri yoyote unatokana na mapato na si vinginevyo.

Awali Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovson Mtangeki, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson aliipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa miaka tisa mfululizo na kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa kada zote za utumishi wakiwamo madiwani na Serikali.

Alisema halmashauri hiyo imekuwa na miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha na kuwa kazi ya ukaguzi ni lazima ifanywe na viongozi wote na si kumuachia mkuu wa wilaya peke yake.

Alisema licha ya kuwepo kwa kamati, wataalam, maafisa kata na tarafa kwa ajili ya kusimamia miradi hiyo katika utekelezaji wake madiwani hawawezi kukwepwa kwa namna yoyote ile ukizingatia kuwa miradi mingi inayofanyika ipo kwenye maeneo yao.

“Mheshimiwa Mwenyekiti nimesimama mbele ya baraza lako hili tukufu kuwaomba madiwani wetu walau wawe wanakwenda kuikagua miradi hiyo mara mbili kwa wiki watakuwa wamesaidia kwani nguvu yao inahitajika sana,” alisema Mtangeki.

Aliwaomba madiwani hao kuilinda,kuisimamia na kuwahamasisha wananchi waweze kushiriki katika utekelezaji wake na itekelezwe kwa wakati na viwango vinavyohitajika.

Katika hatua nyingine Mtangeki aliomba wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo vitu vinavyosaidia ujenzi kama mchanga, mawe na vingine vifikishwe eneo la ujenzi siku moja kabla tofauti na ilivyo sasa ambapo huwa vinapelekwa siku ya kazi jambo ambalo linawafanya mafundi wasifanye kazi kwa ufanisi.

Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Justice Kijazi alisema mwaka wa fedha wa 2023/ 2024 madiwani wote wa halmashauri hiyo watafanya ziara ya mafunzo kwenda Wilaya ya Tanganyika kujifunza namna bora ya utunzaji wa mazingira kutokana na wilaya hiyo kuwa kinara wa utunzaji mazingira hapa nchini.

Hatua hiyo ilifikiwa na Kijazi kufuatia maombi ya baadhi ya madiwani kuomba kufanyika kwa ziara hiyo ambayo itakuwa na tija kwa halmashauri hiyo kwenye suala zima la uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Katika kikao hicho watumishi wa halmashauri hiyo walioongoza kwa ukusanyaji wa mapato akiwepo mratibu wa nyumba za halmashauri hiyo zilizopo Manispaa ya Singida, Jonath Lutiga walipatiwa zawadi ya fedha taslimu kuanzia Sh. 300,000 kama motisha ili kuwafanya kuwa na mori wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live