Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miaka saba ya vuta nikuvute kesi ya Mwale ikimalizika kwa kulipa Sh200 milioni Arusha

30399 MWALE+PIC TanzaniaWeb

Thu, 6 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mwanzoni mwa wiki hii, wakili maarufu jijini hapa, Median Mwale alihukumiwa kulipa faini ya Sh200 milioni au kwenda jela miaka mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya utakatishaji wa fedha.

Hukumu hiyo imekuja ikiwa ni miaka takriban saba tangu ofisa huyo wa mahakama alipojikuta matatani na kushikiliwa mahabusu hadi hukumu ipotolewa.

Katika hukumu hiyo, Jaji Issa Maige wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha pia alimhukumu Mwale kifungo cha jumla ya miaka saba - kifungo ambacho tayari amekitumikia baada ya kukiri makosa ya kula njama, kugushi na kuandaa nyaraka za uongo.

Hata hivyo, hadi juzi taratibu za ulipaji faini zilikuwa zikiendelea, pia mawakili wake wamewasilisha maombi maalumu ya kulipa faini hiyo kidogokidogo wakitumia sababu kuwa kwa muda mrefu Mwale alikuwa akitegemea kazi ya uwakili na kwa miaka saba hajafanya kazi hiyo.

Kukamatwa kwa Mwale

Mwale alikamatwa Agosti 2011 na kufikishwa mahakamani Agosti 19, 2011 na alisomewa mashtaka 13 akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru alikokuwa amelazwa baada ya kuugua akiwa mikononi mwa polisi.

Katika shauri hilo ambalo limekuwa gumzo jijini Arusha, washtakiwa wengine ni mameneja wa benki ya CRDB, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi huku aliyekuwa mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Donbosco Gichana ambaye ni raia wa Kenya alikiri makosa yake na kulipa faini.

Kesi hiyo iliyopitia hatua mbalimbali hadi kufikia Mwale kukiri makosa na kuhukumiwa, ilianza kusikilizwa Novemba 27, 2015.

Ilipoanza kusikiliza kesi hiyo, wakili wa Serikali, Awamu Mbagwa alidai washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Februari 2009 hadi Februari 2011.

Mbagwa alidai katika kipindi hicho Gichana ambaye aliwahi kuishi nchini Marekani alishirikiana na mshtakiwa wa kwanza, Mwale na wenzao kugushi hundi kutoka nchini humo na kuziingiza hapa nchini kupitia akaunti zilizofunguliwa Benki ya CRDB tawi la Meru lililopo mkoani hapa.

Alidai hayo yalibainika kutokana na uchunguzi uliofanywa nchini Marekani na maofisa wa polisi wa hapa nchini ambao walipata vielelezo kadhaa ikiwemo mali zilizonunuliwa kwa fedha hizo, nakala za hundi zilizotumika na mikataba.

Katika mashtaka dhidi ya Mwale, alishtakiwa kwa utakatishaji fedha - kosa ambalo ni kinyume cha Sheria ya Kupinga Utakatishaji Fedha namba 12(d) na 13(a) kifungu cha 12 ya mwaka 2006.

Kwa upande wa Donbosco alisomewa mashtaka ya kugushi na kuhusika na utakatishaji fedha kwa kushirikiana na Mwale.

Kwa upande wao, Mwimbwa na Ndejembi walisomewa mashtaka ya kushiriki kula njama, kugushi na kuhusika na utakatishaji fedha wakishirikiana na watuhumiwa wengine.

Katika shauri hilo wakati huo, upande wa mashtaka ulieleza ulitarajiwa kuita mashahidi 46 na kuwa na vielelezo 60.

Vielelezo kukataliwa

Desemba 18, 2015, Mahakama Kuu ilikataa kupokea vielelezo vitano vya ushahidi kutoka nchini Merekani.

Akisoma uamuzi mdogo wa kesi hiyo, Jaji Gadi Mjemmas alikubaliana na mawakili wa utetezi kuwa baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo havikukidhi sheria.

Alisema mahakama imekubali kupokea kielelezo kimoja cha Anna R Marchison cha hati ya kusafiria - kielelezo ambacho kilithibitishwa na ofisa wa Serikali ya Marekani, John Kerry.

Vielelezo hivyo viliwasilishwa mahakamani hapo na shahidi wa pili upande wa mashtaka, ofisa upelelezi wa polisi makao makuu, Suleiman Nyakulinga.

Jaji Mjemmas alisema kwa kuzingatia sheria inayosimamia taratibu za upatikanaji wa ushahidi na mashahidi nje ya nchi (mutual assistance in crimminal matters act cap254) katika makosa ya jinai ni muhimu vielelezo vifuate sheria.

Alisema kifungu cha 38(2) a na b cha sheria hiyo vinaeleza kuwa nyaraka ambayo itaonekana kukubalika mahakamani kutoka nchi nyingine inapaswa kuwa imesainiwa na jaji, hakimu au ofisa wa Serikali wa nchi husika au kiapo cha shahidi kilichothibitishwa.

Katika uamuzi huyo, Jaji Mjemmas alikubaliana na hoja ya wakili wa utetezi, Omar Omar kuwa Tanzania ni nchi huru, hivyo ni lazima sheria zake zifuatwe katika kufikia uamuzi ingawa pia haiwezi kujitenga na mataifa mengine.

Kufutiwa mashtaka 44

Wakati kesi hiyo ikiendelea, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, David Mrango alitoa uamuzi wa kufuta kesi hiyo Oktoba 3, 2017 baada ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kueleza hana sababu ya kuendelea nayo.

Wakili mwandamizi wa Serikali, Oswald Tibabyekomya ndiye aliyewasilisha hoja ya upande wa mashtaka. Hata hivyo baada ya shauri hilo kufutwa washtakiwa walikamatwa tena wakiwa nje ya viwanja vya mahakama.

Awali, jopo la mawakili wa utetezi waliiomba mahakama isikubali maombi hayo kwa madai kuwa yalilenga kuwatesa wateja wao kwa kuwa haikuwa mara ya kwanza kuachiwa kisha wakakamatwa tena.

Jaji Mrango alisema mahakama haikuwa na mamlaka ya kukataa maombi hayo ya DDP, isipokuwa alisisitiza kuwa endapo upande wa mashtaka wamewasilisha ombi hilo kwa nia njema, basi waondoe shauri hilo na washtakiwa wasikamatwe.

Wakili wa utetezi, Albert Msando akiwasilisha pingamizi hilo, aliieleza mahakama kuwa DPP alitakiwa kutoa sababu za kutoendelea na kesi hiyo kwani alikuwa na muda wa miaka miwili kufanya hivyo, lakini hakufanya hivyo jambo alilodai kuwa ni matumizi mabaya ya sheria.

Alisema wao (upande wa utetezi) walikuwa na taarifa za DPP kuandaa polisi nje ya mahakama kuwakamata tena washtakiwa hao ili kuwafungulia shauri jingine.

Hata hivyo, Wakili Tibabyekomya alipinga hoja hizo kwa madai kuwa sheria haimlazimishi DPP kutoa sababu ya kuondoa kesi mahakamani pindi akiona kuna haja ya kufanya hivyo.

Baada ya majadiliano hayo jaji aliwaachiwa huru washtakiwa hao, lakini wakiwa nje walikamatwa tena na kurejeshwa mahabusu.

Kesi kuanza upya

Baada ya kesi kufutwa na kisha kukamatwa tena, washtakiwa hap walirejeshwa mahakamani Novemba 8, 2017.

Hata hivyo ilishindikana kusomewa mashtaka mapya kutokana na kutowasilishwa kwa jalada la kesi hiyo kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Nestory Baro.

Wakili Mkuu wa Serikali, Hashim Ngole aliomba kesi hiyo iahirishwe kutokana na jalada hilo kuwa Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Novemba 10, 2017 kesi ilianza na upande wa mashtaka ulieleza kuwa unatarajia kuwa na mashahidi 69 na vielelezo zaidi ya 100.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, upande huo ulikuwa ukiwakilishwa na mawakili Tibabyekomya, Pius Hilla, Shedrack Kimaro, Mbagwa na Hashim Ngole uliwasomea washtakiwa hao mashtaka 42 .

Baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo hayo na Wakili Kimaro, Hakimu Barro alisema jalada hilo litapelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa ajili ya kusubiri kupangiwa jaji atakayesikiliza kesi hiyo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haina uwezo wa kuisikiliza.

Mmoja akiri makosa, aachiwa

Septemba 19, mwaka huu, Donbosco alikiri makosa na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela pamoja na kulipa faini ya Sh300 milioni.

Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Issa Maige na kwa kuwa mshtakiwa alikuwa tayari amekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka mitano, alilipa faini ya Sh300 milioni na kuachiwa huru.

Mwale akiri, ahukumiwa

Baada ya Septemba 24, washtakiwa watatu akiwamo Mwale, Mwimbwa na Ndejembi kusomewa mashtaka 59, iliahirishwa ambapo mawakili wa washtakiwa; Omari Omari, Emmanuel Mvula na Innocent Mwanga hawakuzungumza lolote juu ya mashahidi waliowaandaa.

Kesi hiyo ilipokuja Novemba 28, mbele ya Jaji Maige, Mwale alikiri makosa na hukumu dhidi yake ilitolewa mwanzoni mwa wiki hii na aliamriwa kulipa faini ya Sh200 milioni na kifungo cha miaka mitano gerezani.

Hata hivyo kwa kuwa amekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka saba, atapaswa kulipa faini na hadi jana alikuwa bado hajakamilisha ulipaji wa faini hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz