Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhudumu wa hoteli mwenye ndoto ya kuwa mhandisi wa umeme

48462 Pic+mhudumu

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Umri wa miaka 27 na mwonekano wake unatosha kumtambulisha kuwa binti. Ni mpole, mkarimu na kipenzi cha watu.

Elizabeth David, mhudumu wa hoteli msomi wa fani ya mifumo ya umeme wa majumbani daraja la tatu mwenye ndoto ya kuwa mkurugenzi wa kampuni ya uuzaji wa vifaa na mhandisi wa umeme.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Elizabeth ambaye anaishi Manzese Bakhresa jijini Dar es Salaam, anasema hapendi kufanya kazi ya uhudumu wa hoteli lakini ukosefu wa ajira ndicho chanzo cha yeye kufanya shughuli hiyo.

“Sipendi kufanya kazi hii. Hata hivyo, sitegemei kuifanya maisha yangu yote, ndoto yangu ni kumiliki kampuni yangu na kujiendeleza kielimu hadi niwe injinia rasmi wa umeme wa majumbani. Hii ndiyo kazi niipendayo toka moyoni.

Elizabeth anasema ni mzaliwa wa pili kati ya watoto sita wa familia ya Neema Emmanuel na David Emmanuel na ndiye tegemeo la familia kwa sasa.

“Nimezaliwa mkoani Mwanza katika wilaya ya Ilemela, mtaa wa Mabatini, elimu ya msingi nimesoma katika Shule ya Msingi Mabatini kuanzia mwaka 2001 hadi 2007, elimu ya sekondari nimeipata katika Shule ya Sekondari Mwanza kuanzia mwaka 2008 hadi 2011,” anasema.

Baada ya hapo Elizabeth anasema alijiunga na masomo ya ufundi wa umeme katika chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Mwanza mwaka 2012 hadi 2014 na kuhitimu daraja la tatu katika fani ya ufundi wa umeme majumbani (instoletion).

“Nilikuja Dar es Salaam mwaka 2015 baada ya kuitwa kwenye usaili wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) baada ya kutuma maombi ya kazi,” anasema.

“Sikufanikiwa kupita katika usaili huo. Nikaona siyo vyema kurudi nyumbani (Mwanza), kwa kuwa nina ndugu zangu hapa Dar es Salaam basi nikae nitafute utaratibu mwingine wa kupata kazi,” anasema.

Anasema aliamua kutafuta kazi akapata ya uhudumu wa baa, lakini hakufurahishwa nayo kutokana na namna watu wanavyowachukulia wahudumu wa baa, manyanyaso na mishahara midogo,” anasema.

Anasema aliamua kuachana na kazi hiyo na kutafuta nyingine ambapo alipata ya kuhudumia hotelini ambayo anaendelea nayo na inamwezesha kuendesha maisha yake ikiwamo kula, kuvaa na kulipa kodi ya nyumba.

Mbali na kazi hiyo, pia Elizabeth mara nyingi hufanya vibarua mtaani vya kutengeneza mifumo ya umeme wa majumbani akiongozana na wahandisi wanaotambulika ambao humuita pale zinapojitokeza kazi za muda mfupi.

“Nina mwaka wa tatu sasa nahangaikia kupata kazi Tanesco kila maombi yakitoka ninatuma, lakini ninakosa. Nahisi zile nafasi za ajira hutangazwa kama uthibitisho tu...,” anasema.

“Nakumbuka kuna siku nilikwenda pale Tanesco nikakutana na mama mmoja mapokezi akanitaka nimpe vyeti na barua zangu za maombi. Alichokifanya alichukua akafungua bahasha akaniuliza barua ya kazi inaandikwa hivi? Akanitupia chini. Niliumia sana,” anasema.

Elizabeth anaeleza kuwa pamoja na hayo, hajakata tamaa anaamini ipo siku atatimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi wa umeme wa majumbani.

“Sipendi watu wanaowadharau wenngine na hasa wanaowadharau wahudumu wa baa na hotelini kwa kuwaona si kitu. Wakae wakijua kuwa si kila ‘baamedi’ ni muhuni au hajasoma wapo waliokwenda shule na wanaojielewa,” anasema.

Elizabeth anasemba katika maisha yake anapenda haki na kuchukia uonevu au manyanyaso dhidi ya binadamu mwenzake, anapenda kuelezwa ukweli hata kama ni mchungu.

“Sipendi kudanganywa, huwa ninaumia ikitokea nimedanganywa na huwa ninapata amani mtu akiniambia ukweli hata kama ni mchungu,” anasema.

Elizabeth anasema anavutiwa na utendaji wa Rais John Magufuli kwani ni kiongozi ambaye amewafundisha watu kufanya kazi ili wapate kula. “Huo ndiyo ukweli, japo wapo wanaomkosoa lakini kwangu ni kiongozi bora atakayeifikisha nchi yetu mbali,” anasema.



Chanzo: mwananchi.co.tz