Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhubiri wa Kenya azusha sintofahamu Arusha

Mhubiri Pic Kenya Arusha Mhubiri wa Kenya azusha sintofahamu Arusha

Fri, 14 Jul 2023 Chanzo: mwanachidigital

intofahamu kati ya viongozi wa Jiji la Arusha na wananchi imeibuka baada ya kutolewa kibali cha kufanya mkutano wa injili kwa mhubiri, Ezekiel Odero ambaye ni kiongozi wa Kanisa la New Church of Kenya.

Mhubiri huyu anatajwa kuwa mfuasi wa mhubiri Paul Mackenzie, aliyesababisha vifo vya waumini wake zaidi ya 300 nchini Kenya.

Mhubiri huyo akishirikiana na mhubiri Mtanzania, Soni Nabii ametoa matangazo kuwa atafanya mkutano mkubwa uliopewa jina “siku tatu za kubadilishwa na Mungu jijini Arusha” kuanzia leo hadi keshokutwa katika Uwanja wa shule ya msingi

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo alisema hana taarifa kuhusu mkutano huo wa injili.

“Sina taarifa za ujio wa huyo mhubiri, lakini baada ya hizi taarifa tutalifuatilia, nitatuma askari huko Ngarenaro kufuatilia zaidi,” alisema.

Odero ni mshirika wa mhubiri Paul Mackenzie wa Kenya ambaye kati ya Machi na Juni mwaka huu, anatuhumiwa kusababisha vifo vya waumini wake zaidi ya 300 kutokana na mafundisho ya kiimani kwa kuwataka wafunge hadi kufa ili kukutana na muumba wao.

Miili ya waumini hao ilibainika baada ya jeshi la polisi la Kenya kutafuta na kufukua makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola uliopo karibu na mji wa pwani wa Malindi, waathiriwa wa kwanza walifariki na wengine walikutwa hai wakiwa dhoofu.

Ofisa utamaduni wa jiji la Arusha, Lucy Jilanga alisema wametoa kibali cha kufanyika mkutano wa injili wa siku tatu katika viwanja vya shule ya Ngarenaro wiki hii.

“Wewe jua kibali kimetolewa wafanye mkutano wa injili basi, hayo mengine wewe yanakuhusu nini,” alihoji ofisa huyo na kukata simu baada kuulizwa kama ana taarifa za mchungaji Odero kutajwa kwenye tuhuma vifo vya waumini nchini Kenya.

Hata hivyo, diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita alisema hawatambui kibali walichopewa wahubiri hao.

“Baada ya kupata taarifa za haya mahubiri, mimi nilimtuma mtendaji wangu wa kata kufuatilia hadi polisi na tukaambiwa hawana taarifa na hawajatoa kibali,” amesema.

Alisema baadae aliwasiliana na uongozi wa shule, hata hivyo nao hawakuwa na taarifa licha ya kiwanja hicho kuwa katikati ya shule ya msingi Ngarenaro na sekondari ya Mgarenaro.

“Sijui kinachoendelea kwani hivi sasa shule zina mitihani, kuruhusu haya mahubiri tena mhusika mmoja anatajwa katika kesi kwao si sawa,” amesema.

Diwani, Doita ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya madiwani ya maendeleo ya jamii, alisema tayari jiji limetoa kibali na wao kama kamati ya maendeleo ya kata hawatakubali mahubiri hayo.

“Hili siyo sawa, inaonekana waliotoa kibali wala hawamjui huyu mhubiri kwa sababu kumbukumbu zetu zimeleta shida Kenya lakini mimi nitaendelea kuzungumza na viongozi wengine kusitisha kibali,” amesema.

Naye Raphael Lemuya, mkazi wa Ngarenaro alisema atashangaa kama mhubiri Odero atapewa kibali hicho.

“Sisi kama majirani na uwanja, tumeona matangazo, kweli tumeshangaa lakini tunajua hawa wana fedha za kufanya lolote, hivyo sintashangaa wakipewa kibali,” amesema.

Hata hivyo, hakuna mwalimu wa shule ya msingi Ngarenaro ama sekondari ambaye alikuwa tayari kuzungumza kwa maelezo msemaji ni Mkurugenzi wa jiji la Arusha.

Jana mchana, juhudi za kuwapata wahubiri hao zilikwama na haikujulikana wako wapi licha ya kuonekana baadhi ya waumini wakianza maandalizi ya jukwaa.

Jeshi la polisi mkoa Arusha, pia limeeleza kwamba bado halina taarifa sahihi kuhusiana na mkutano wa wahubiri hao.

“Wanaotoa vibali ni wilaya, sasa kama wao wamemwambia diwani wa Ngarenaro hawana taarifa na hapa mkoani sidhani kama zipo,” amesema ofisa wa polisi mkoa Arusha.

Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Justine Masejo hakupatikana jana kwenye simu yake ya mkononi ili kuelezea sintofahamu hiyo.

Chanzo: mwanachidigital