Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhasibu wa CWT adaiwa kujinyonga chooni ofisini

Katembo1 Ed Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Nikodemus Katembo

Thu, 7 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mhasibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara ambaye ni Mratibu Elimu Kata, Kata ya Matawale, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Angelus Mwinyuku (46) amefariki dunia, akidaiwa kujinyonga katika choo cha ofisi ya chama hicho kwa kutumia kamba ya manila.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Nikodemus Katembo, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wilayani Masasi katika ofisi ya CWT iliyoko Mtaa wa Wapiwapi, Kata ya Nyasa.

Alieleza kuwa mwili wa mhasibu huyo ulikutwa chooni ukining'inia kwenye kamba hiyo ya manila iliyofungwa katika dirisha.

Alisema kuwa baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za tukio hilo, lilifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kushuhudia na kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Kamanda Katembo alisema sababu za mhasibu huyo kujinyonga bado hazijajulikana. Uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa na jeshi hilo.

Alisema Jeshi la Polisi litatoa taarifa kuhusu chanzo cha kifo cha mhasibu huyo baada ya kukamilisha uchunguzi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Masasi, Salumu Gembe alithibitisha kupokea mwili wa mhasibu huyo juzi saa moja usiku na kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.

Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Masasi, Thabiti Thabiti, alisema chama hicho kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo hicho. Kinatoa pole kwa ndugu na jamaa wa mhasibu huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live