Wafanyakazi na vibarua zaidi ya 300 wanaofanya kazi ya Ujenzi katika Mradi wa Barabara ya Mabasi ya mwendo wa haraka eneo la Mbagala wamegoma kufanya kazi na kutelekeza vifaa vya kazi barabarani hadi hapo madai yao yatakapotekelezwa.
Miongoni mwa madai ya Wafanyakazi hao waliogoma kufanya kazi ni pamoja na Malimbikizo ya fedha za Chakula, Nauli pamoja na kodi ya pango ambazo zilitakiwa kujumuishwa katika Mishahara yao lakini kwa zaidi ya miaka miwili fedha hizo hawajazipata.
Madai mengine kwa mujibu wa maelezo ya wafanyakazi hao ni pamoja na usalama kazini ambapo wanadai kuwa baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakiumia kazini na uongozi kushindwa kuwahudumia huku wengine wakifukuzwa kazi bila sababu za msingi.
Kiongozi wa Wafanyakazi hao ambaye anadai kufukwa kazi kwa kile anachodai bila sababu za misingi amesema pamoja na viongozi kadhaa kufika na kukutana na uongozi lakini bado ufumbuzi wa malalamiko yao hayajapatikana.
Wanahabaru walifanya juhudi ya kutaka kuuona uongozi wa kampuni hiyo unaohusika na wafanyakazi, lakini baadhi ya walinzi waliokuwa eneo hilo waligoma kutoa ushirikiano na kusema kuwa afisa anayewasimamia wafanyakazi hakuwepo ofisini.
Mgomo wa wafanyakazi hao umekuwa ukiibuka Mara kwa mara ambapo mwanzo mwa Januari mwaka huu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe aliingilia kati na kutoa mwongozo na katikati ya Agosti, Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo alitoa Siku 14 kwa Uongozi kushughulikia Mgogoro huo, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.