Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgomo wa daladala Moshi wazidi kuleta machungu

Wed, 5 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi.  Mgomo wa daladala mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ulioingia siku ya tatu leo Jumatano Desemba 5, 2018, umesababisha kupanda kwa nauli za Bajaj.

Mgomo huo wa daladala kupinga Bajaj kupakia abiria katika vituo vya mabasi umesababisha Bajaj kupandisha kiwango cha fedha wanachowatoza abiria kutoka Sh500 hadi 1,000.

Daladala ambazo hazitoi huduma tangu Jumatatu Desemba 3, 2018 ni zile zinazotoa huduma ya usafiri kati ya Moshi mjini na KCMC, Majengo, Soweto na Pasua.

Baadhi ya wanafunzi, wafanyakazi na wafanyabiashara sasa wanalazimika kutembelea umbali mrefu kutokana na kukosa usafiri na kukwepa kutumia usafiri mbadala.

Mwanafunzi wa shule ya msingi Majengo mkazi wa Msaranga , Dorine Gerald amesema, "Huu mgomo umetuathiri tunatembea kutoka Kata ya Msaranga hadi majengo. Tukifika shule wengi tunakuwa tumechoka. Tunalipa Sh200 katika daladala lakini waendesha Bajaj hawataki tupande, pia bei yao ni kubwa.”

Mkazi mwingine wa jijini humo, Amani Tesha amezitaka malaka husika kuingilia kati kwa maelezo kuwa Sumatra imeshindwa kusimamia suala hilo.

Innocent Kimario, dereva wa daladala amesema ni ajabu kuona viongozi wa manispaa ya Moshi wakitoa matamko bila utekelezaji.

“Jumatatu wiki hii walikutana na viongozi wetu, wakazungumza  na kuahidi kuwa watapita maeneo husika kwa ajili ya kutoa matangazo ya kuwaondoa wenye Bajaj lakini mpaka leo ni siku ya tatu hakuna kinachoendelea,” amesema Tesha.

“Hawa madereva Bajaj wameshaelezwa kutosimama katika vituo vyetu vya mabasi lakini hawasikii. Sisi pia tuna familia zetu tunatakiwa kujiingizia kipato kwa kazi hii ya daladala sasa kama hatupakii abiria wote wanakwenda kwenye Bajaj tunaishije?”

Jana ,Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya alilieleza Mwananchi kuwa madereva wa daladala na Bajaj wanatakiwa wakae wakubaliane namna ya kuondoa changamoto hiyo kwa maelezo kuwa mji huo ni mdogo na Bajaj haziwezi kuondoka katikati ya mji.

Soma zaidi: Mgomo daladala ngoma mbichi



Chanzo: mwananchi.co.tz