Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgomo daladala ngoma mbichi

Wed, 5 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Vuta nikuvute ya mgomo wa madereva wa daladala mjini Moshi imeendelea kuwaumiza vichwa wananchi kutokana na adha ya usafiri wanayokumbana nayo.

Mgomo huo ambao ulianza juzi bado haujapatiwa ufumbuzi licha ya viongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Manispaa ya Moshi kuitisha vikao na viongozi wa wamiliki daladala na Bajaj ili kusaka suluhu ya mgomo huo.

Daladala zilizogoma kusafirisha abiria ni zile zinazofanya safari zake kati ya Moshi Mjini na KCMC, Majengo na Soweto. Wakizungumzia kadhia ya usafiri, baadhi ya wakazi wa Moshi walisema mgomo huo umewaathiri hata baadhi ya wanafunzi ambao walishindwa kwenda shuleni kwa wakati.

Mwanafunzi Jackline Mroso, anayesoma Shule ya Sekondari Majengo aliliambia Mwananchi kuwa kutokana na mgomo huo, pamoja na wenzake walilazimika kutembea umbali mrefu ili kufika shuleni.

“Kilichoniokoa ni kwamba alikuja msamaria mwema akanipa lifti, lakini jana (juzi) tumelazimika kutembea umbali mrefu,” alisema Jackline.

Mfanyabiashara wa Msaranga, Agatha Joseph alisema alikwama kwenda sokoni kununua bidhaa kutokana na mgomo huo. Mkazi wa Moshi mjini, Amina Saleh alisema, “Sasa hawa (daladala) wanaofanya mgomo waendelee, ujio wa Bajaj kwa hapa mjini ni msaada mkubwa.”

Kiongozi wa madereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Moshi mjini na KCMC, Ibrahim Mzava alisema katika kikao chao kilichofanyika juzi mchana na uongozi wa Manispaa ya Moshi pamoja na Sumatra, walikubaliana kuziondoa Bajaj hizo jana, lakini hakuna kilichotekelezwa hadi jioni.

“Jana (juzi) walituambia baada ya kile kikao watapita na gari la matangazo kutangaza kuziondoa Bajaj hizo mjini, (lakini) hawajafanya hivyo. Tumeamua kupaki tena, hatufanyi kazi mpaka kieleweke,” alisema.

Kiongozi wa waendesha Bajaj, Rashid Omari alisema walichokubaliana kikaoni ni kuwa Bajaj zitaendelea kufanya kazi katikati ya mji, lakini hazitasisimama kwenye vituo vya daladala. “Wacha wao waendelee na mgomo lakini kinachotakiwa hapa ni kufuata sheria zilizowekwa na Bajaj zetu ziendelee kupiga kazi kama kawaida,” alisema Omary.

Hata hivyo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymound Mboya alisema mji huo ni mdogo na kinachotakiwa ni wahusika kuwa na busara zaidi.

Alisema kuziondoa Bajaj katikati ya mji haitawezekana kwa sababu nazo zinafanya biashara na wahusika wanamiliki leseni za usafirishaji.



Chanzo: mwananchi.co.tz