Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgogoro wasababisha Dar kutapakaa taka

33750 Pic+mgogoro Tanzania Web Photo

Fri, 28 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Halmashauri mbili za Jiji la Dar es Salaam zimeingia katika mvutano na wakandarasi wa uzoaji takataka hali inayosababisha maeneo hayo kukithiri kwa uchafu.

Halmashauri hizo ni za Ubungo na Kinondoni ambazo ukipita maeneo mbalimbali utashuhudia mrundikano wa takataka barabarani na karibu na makazi ya watu kutokana na kutozolewa.

Wakandarasi hao wamelalamikia utaratibu mpya ulioanzishwa na halmashauri hizo kuchukua sehemu ya mapato yatokanayo na ukusanyaji wa takataka mitaani.

Katibu wa Chama cha Wakandarasi wa Takataka – Sinza, Stephano Lukinga jana alisema mabadiliko hayo yamefanyika bila kuwashirikisha na kwamba kazi yao ni ngumu na inatumia fedha nyingi.

“Sasa tunaambiwa kwamba watendaji watakuwa wanakusanya fedha za takataka, kisha asilimia 20 zinakwenda Manispaa na asilimia 10 zinabaki kwenye Serikali za mitaa. Sisi tunaitambua hiyo asilimia 10 ya Serikali za mitaa lakini hiyo 20 iliyoongezeka inatuumiza,” alisema.

Mkandarasi mwingine kutoka Kikundi cha Umoja wa Faraja, Forastina Ndoroki alisema wao wanakodi magari moja kwa Sh400,000 kuzoa taka ukiacha gharama nyingine za wafanyakazi.

Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema fedha yoyote inayokusanywa kwa wananchi ni ya umma, hivyo Serikali ina jukumu la kukusanya fedha hiyo na kutumia kwa malengo kusudiwa.

“Maduhuri yote yanakusanywa na Serikali, kama wao wanalipwa fedha zao kwanini waachwe wakusanye wenyewe,” alisema.

Kuhusu wakandarasi kutoshirikishwa kwenye mabadiliko hayo, mkurugenzi huyo alisema: “Wao (wakandarasi) wanatafuta kazi, kwanini washirikishwe? Ukiomba kazi ukapewa, ushirikishwe nini tena?”

Mkurugenzi wa Ubungo, Beatrice Kwai alisema hawezi kuzungumza kwa sababu hayupo ofisini na alipotafutwa pia juzi alisema asingeweza kuzungumza kwa sababu alikuwa kanisani kwenye shughuli ya ubatizo.



Chanzo: mwananchi.co.tz