Mgogoro baina ya wakulima na wafugaji unaoendelea katika Kata ya Lunguza, Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, umechukua sura mpya baada ya wakulima kuwaua baadhi ya ng'ombe kwa kuwakatakata na kuwatenganisha viwiliwili na vichwa.
Hali hii ilitokea jana Jumanne, Novemba 5, 2024 baada ya mifugo hiyo kuingia kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu hekta 100 za mazao yao mbalimbali. Ng’ombe wawili walikutana na kadhia hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 6, 2024 amesema mgogoro huo umezusha taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Kamanda Mchunguzi amesema polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini watuhumiwa waliohusika na uharibifu huo na hatua za kisheria zitachukuliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye amewataka wakulima na wafugaji kukaa chini na kujadiliana ili kutafuta suluhu ya kudumu kwa mgogoro huo, ambao haufai kwa jamii.
Sumaye amesisitiza wananchi wanapaswa kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake, wafugaji wanapokamata mifugo inayoingia kwenye mashamba yao na kuharibu mazao, wanapaswa kuipeleka mifugo hiyo kwa vyombo husika.
"Mkulima anapaswa kulima kwenye maeneo yake, na mfugaji afuge kwenye maeneo yake," amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Mwananchi wa kijiji cha Lunguza, Alen Shemmela amesema mgogoro huo ni wa muda mrefu ambao unawapa changamoto kubwa sababu haumaliziki licha ya kutafuta suluhu kupitia viongozi wa ngazi ya juu.
"Sisi kama wazee tuliwahi kuandika barua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Chama Wilaya na tulipeleka barua hadi kwa mkuu wa mkoa na alishafika hapa na mgogoro haujaisha bali sisi wakulima mazao yetu yanaliwa," amesema Shemmela.
Taraka Kei ni mfugaji wa eneo hilo la Lunguza amesema ili kupata suluhu ya kumaliza mgogoro huo ni kukaa wazee wa pande zote mbili pengine mgogoro unaweza kuisha.