Arusha. Mgogoro wa kugombea mwili wa mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Jubilate Ulomi ambao unafikisha siku ya nane bila kuzikwa, umechukua sura mpya baada ya kufikishwa mahakamani.
Mwili wa mchimbaji huyo anayemiliki migodi kitalu B, Mirerani wilayani Simanjiro, umefikishwa mahakamani siku moja baada ya mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kushauri kusitishwa kwa mazishi ili haki ikatafutwe mahakamani. Sabaya alitoa uamuzi huo, baada ya kukutana na pande zote zinazohusika za mgogoro huo.
Kikao hicho, kilichochukua zaidi ya saa tatu na kilichojumuisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, hakikuweza kufikia maridhiano.
Akizungumza na Mwananchi, Zainabu Rashid ambaye ni mke wa Jubilate waliyezaa naye watoto wawili, alisema ameamua kufikisha mgogoro huo mahakamani ili apate haki yake na watoto.
Zainabu alisema anaamini haki itatendeka mahakamani, akitaka kuwekwa wazi kwa utaratibu wa mirathi ya mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki nyumba za kifahari na magari.
Alisema awali hakushirikishwa na wanafamilia walikuwa wamemteua Werandumi Olomi kusimamia mirathi.
Ndugu wa Zainabu aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema wanachosuburi ni kupangiwa hakimu na siku ya kuanza kusikilizwa.
“Tutatoa taarifa kamili baada ya kupata tarehe ya kesi, lakini ambacho ninaweza kusema sasa tayari suala hili tumelifikisha mahakamani,” alisema.
Zainabu pia anaomba ufanyike uchunguzi wa kifo cha mumewe ili kujua chanzo, akidai kuwa hakupewa taarifa za kuumwa kwake na kupelekwa Nairobi alikofia.
“Nilipata wasiwasi kwa nini wanataka kwenda kumzika mume wangu haraka na kwa nini wananizuia?” alisema.
“Lakini pia wamezuia mali zote za marehemu yakiwemo magari na nyumba ambayo wameifunga na hawataki mwili kupelekwa kuagwa nyumbani kwake Mirerani.”
Jubilate alifariki dunia Januari 15 katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kupelekwa kwa matibabu na hadi leo mwili wake umefadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Hai.