Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgogoro wa familia wasababisha ekari 11 za mahindi kuharibiwa

Uharibifu Mashambaniii.png Mgogoro wa familia wasababisha ekari 11 za mahindi kuharibiwa

Thu, 21 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mgogoro wa familia mbili katika Kijiji cha Halungu wilayani Mbozi umesababisha ekari 11 za shamba la mahindi kuharibiwa kwa kupuliziwa dawa ya kuua magugu.

Tukio hilo limetokea Desemba 18, 2023 katika Tarafa ya Itaka mkoani Songwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya amethibitisha tukio hilo leo Desemba 21,2023 alipozungumza na waandishi wa habari akisema ekari 11 za shamba la mahindi zimeharibiwa kwa kupuliziwa dawa ya kuua magugu na watu ambao hawajajulikana wanaoendelea kutafutwa.

New Content Item (1) New Content Item (1)

Amesema shamba hilo limelimwa na watu wanne waliolikodi kwa Edina Mgala.

Kamanda Mallya amesema Edina alikodisha shamba hilo kwa kuligawa kwa watu hao ambao ni Mailo Msangawale (35) aliyekodi ekari saba, Emi Magwaza (48) alikodi ekari 1.5,

Salome Nkota (50) alikodi ekari 1.5, na Jeremia Ngoya (42) aliyekodi ekari moja.

Amesema wote wanne ni wakulima na wakazi wa Halungu.

“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi unaohusisha familia mbili kati ya watoto wa mke mkubwa na mke mdogo wa marehemu Focus Makonongo,” amesema Kamanda Mallya.

Amesema polisi Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na maofisa kilimo wilayani Mbozi wanafanya tathimini kujua thamani halisi ya mali iliyoharibiwa na kemikali iliyotumika kufanya uharibifu huo.

“Polisi linatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mtu au watu ambao wamehusika katika tukio hilo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.

Kamanda Mallya ametoa rai kwa wananchi kutokujichulia sheria mkononi, badala yake kutatua migogoro kwa kukaa vikao na kusuluhisha kwa amani.

Salome Nkota, ambaye shamba lake limeharibiwa amesema alipokodi hakujua kama kuna mgogoro. Amesema alipanda mahindi kwa ajili ya chakula na biashara.

“Asilimia kubwa shamba hilo nilikuwa nikilitegemea kwa ajili ya mazao ya chakula na biashara, kitendo kilichofanywa na watu waliopuliza dawa si cha kiungwana. Naomba Serikali iwasake popote walipo na hatua zichukuliwe,” amesema.

Amesema ameingia gharama kubwa za kuandaa shamba, kununua mbegu na pembejeo lakini mwisho wa siku mazao yameharibiwa pasipo watu kuwa na hofu ya Mungu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Halungu, Hezeron Mshani amesema mashamba hayo yaliharibiwa usiku.

“Licha ya marehemu mume wao kuacha wosia, bado mashamba hayo yalikuwa na mgogoro wa muda mrefu wa familia kati ya watoto wa mama mdogo na mkubwa,” amesema.

Amesema wameshughulikia mgogoro huo hadi ngazi ya baraza la ardhi ili kupata suluhisho lakini limetokea tukio la mahindi kuharibiwa.

Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Halungu, Fredy Kasekwa amesema baada ya kupata taarifa ya uharibifu huo, walifika kwenye mashamba na kukuta baadhi ya makopo yenye mabaki ya dawa ya Roundup yakiwa yametelekezwa.

“Bado haijafahamika ni watu gani waliohusika na tukio hilo kwa sasa tumeliachia Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live