Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgogoro wa ardhi Manyara watatuliwa na mawaziri nane

Mgogoropicnnmmn Mgogoro wa ardhi Manyara watatuliwa na mawaziri wanane

Sat, 9 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mawaziri wanane wamefika mkoani Manyara na kutoa taarifa ya Serikali kuridhia baadhi ya wananchi wa vijiji vya Kimotorok Wilayani Simanjiro na Irkiushibor Wilayani Kiteto waliopo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero kupewa makazi rasmi.

Ekari 4,392 zimemegwa na kupatiwa wananchi wa Kata ya Loiborsiret, kijiji cha Kimotorok na vitongoji vya Alikasubai na Kisonoko wilayani Simanjiro na kata ya Makame, kijiji cha Irkiushibor, vitongoji vya Iluchura-Maasasi, Impopong na Loobenek wilayani Kiteto.

Hatua hiyo imepokelewa na wananchi wa maeneo hayo kwa furaha kubwa hivyo kutatua na kuhitimisha mgogoro wa muda mrefu wa Jamii ya wafugaji wa maeneo hayo na hifadhi ya Tarangire na pori la Mkungunero.

Uamuzi huo umetangazwa wilayani Simanjiro na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kisekta ya Mawaziri wanane wanaoshughulikia migogoro 975 nchini.

Lukuvi amesema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kumaliza migogoro yote ya ardhi ambayo inachangia kuvunjika kwa amani ndiyo sababu wamefika eneo hilo.

Amesema Rais Samia ameridhia maeneo hayo ya yarasimishwe kuwa makazi ya wananchi ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa kila mara wa wafugaji na hifadhi. Advertisement

Mbunge wa jimbo la Kiteto, Edward Ole Lekaita amesema serikali ya awamu ya sita imefanya jambo kubwa kwa jamii ya eneo hilo baada ya kuwarudishia wananchi maeneo hayo.

Mbunge mstaafu wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya amesema anamshukuru Mungu kazi nzuri waliyoianza imetekelezwa na Rais Samia.

"Tulishabaini matatizo yote na kazi iliyobaki ilikuwa ni kuja kutamka na serikali ya CCM imekuwa ya waungwana kwa kiasi kikubwa kisichoelezeka," amesema Ole Millya.

Mkazi wa kijiji cha Irkiushibor, John Sau ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa urasimishwaji huo na kupongeza maamuzi hayo

Mkazi wa kijiji cha Kimotorok, Daniel Melau ameahidi kuendelea kutunza mazingira ya maeneo hayo ikiwemo kutokata miti hovyo.

Chanzo: mwananchidigital